Rafiki yangu mpendwa.

Licha ya maisha kuwa magumu, bado watu huwa wanachagua kuyafanya kuwa magumu zaidi. Na wanafanya hivyo kwa kukazana kufanya vitu ambavyo vipo kabisa nje ya uwezo wao au kutaka kubadili vitu ambavyo hawawezi kuvibadili.

Rafiki, kuna nyakati, wewe mwenyewe bila ya kujua, unakuwa umechagua kuwa mtumwa wa watu wengine, bila hata ya wao wenyewe kujua kama umekuwa mtumwa wao.

Chukua mfano, labda ulikuwa unataka kuvuka barabara, mara ghafla inatokea gari ambayo inakwenda kwa mwendo wa kasi sana, na inabaki kidogo tu gari hiyo ikugonge, unakimbia na kusalimika, gari ile inaendelea na kasi yake bila hata ya kusimama. Siku nzima utakuwa unazungumzia tukio hilo, ni jinsi gani watu wasivyo na utu, jinsi gani isivyo salama kupita barabarani. Kwa siku nzima, kila unayekutana naye utamweleza tukio hili. Lakini yule aliyekuwa anaendesha gari ambayo umenusurika kugongwa, hana hata habari, huenda hata hajui kama amenusurika kumgonga mtu, alikuwa na haraka zake na hajui nini kimeendelea kwa wengine kwa haraka zake hizo.

vitabu softcopy

Mfano mwingine ni labda mtu amefanya jambo ambalo wewe limekuudhi sana, jambo ambalo hukutegemea afanye. Lakini anaonekana kutokujali kuhusu hilo alilofanya, wewe linakuumiza sana na muda wote unafikiri kwa nini mtu huyo hajali kabisa. Kila unapomwona unakumbuka alichofanya, kila mtu unamwambia kuhusu alichofanya, lakini yeye mwenyewe hujawahi kumwambia. Unakuwa unafikiri anajua alichofanya, kumbe unakuta hajui kama alichofanya kilikukwaza. Wewe unaendelea kuumia na kuteseka wakati mwenzako anaendelea na mambo yake.

Rafiki, kwa mifano hiyo miwili, unaweza kuona ni jinsi gani ambavyo umewahi kujiweka kuwa mtumwa wa watu wengine, bila wewe kujua na bila wao kujua.

Unapotumia muda wako mwingi kufikiria vitu ambavyo watu wamefanya na havijawa sawa kwako, bila ya kuwaambia wao wenyewe, unajiumiza wewe mwenyewe wakati wenzako wanaendelea na maisha. Unapofikiria kwamba kila mtu anaelewa na kupata hisia kama unazopata wewe, unajidanganya na kujiweka chini ya utawala wa wengine.

Usikubali kuwa kwenye hali kama hii, ni kuchagua kupoteza kabisa furaha yako kitu ambacho hakitakuwa na msaada kwako.

Kama mtu amefanya kitu ambacho hakijawa kizuri kwako, hakikisha unamweleza kwamba alichofanya hakikuwa kizuri kwako na baada ya hapo achana na kitu hicho na songa mbele na maisha yako. Na kama huwezi kumpata mtu huyo kumweleza, basi achana na mawazo hayo mara moja. Jifunze kile muhimu cha kujifunza lakini usiendelee na mawazo hayo kwa muda mrefu.

SOMA; Fanya Mambo Haya 18 Pekee Na Mwaka 2018 Utakuwa Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

Hakikisha wakati wote unakuwa huru, kuanzia kwenye mawazo yako, hisia zako na hata matendo yako. Pasiwepo na mtu yeyote ambaye anakunyima amani kwa kile alichofanya au tabia alizonazo. Kama mtu amefanya kitu usichopenda au usichotegemea, mweleze wazi kuhusiana na hilo kisha songa mbele.

Muda tulionao ni mchache, nguvu zetu zina ukomo na tuna mengi ya kufanya ili kuboresha maisha yetu. Kupoteza muda na nguvu zetu kwa sababu ya mambo waliyofanya wengine, huku tukiwa hata hatujawaambia nini wamefanya, ni kuchagua kuwa chini ya utawala wa wengine, kitu ambacho hakitatusaidia.

Uhuru ni kuchagua na upo huru kwa kadiri unavyoweza kuchagua namna gani unayaendesha maisha yako. Na usikubali kabisa awepo mtu yeyote ambaye anakuzuia wewe kuendesha maisha yako unavyotaka kuyaendesha, hata kama amefanya nini. Kutumia muda wako kuwafikiria zaidi wengine ni kujionea na kujinyima muda unaohitaji ili kuweza kuwa na maisha bora.

Wewe ni kiumbe huru, uliyezaliwa ukiwa huru na umeweza kujenga fikra zako huru, linda uhuru wako huo kwa kutoruhusu wanachofanya wengine, kiwe kizuri au kibaya kikufanye uwafikirie wao tu muda wote. Hapo unakuwa umechagua kuwa mtumwa wa wengine, bila ya wao au wewe mwenyewe kujua.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha