Zipo njia nyingi sana za kuwapoteza wateja kwenye biashara yako. Na kwa njia zote, wewe mwenyewe ndiye unayechagua kuwapoteza wateja. Kuna mambo unakuwa umefanya au kutokufanya, ambayo yanachangia wateja kuondoka kwenye biashara yako.

Japokuwa njia nyingine ni ngumu kwa upande wako, yaani zikishaanza unaweza usiweze kuzuia kwa haraka, zipo njia ambazo ni rahisi sana na umekuwa unatumia kuwapoteza wateja wa biashara yako.

Moja ya njia hizo rahisi ni wateja kukosa uhakika na biashara yako. Pale wateja wanapotaka kitu kwenye biashara yako lakini wanakikosa, kitu ambacho uliwaahidi watapata, wanaanza kukosa imani na biashara yako. wanapokuja wakati mwingine na wakakosa, basi wanajifunza kwamba biashara yako siyo ya kutegemea, hivyo hakuna haja ya kujisumbua kuja hapo, kwa sababu hawana uhakika wa kupata wanachotaka.

SOMA; BIASHARA LEO; Wateja Wako Wanatamani Sana Kitu Hichi Kimoja Kutoka Kwako…

Kazi yako kuu kama mfanyabiashara ni kuhakikisha mteja anapata kile ambacho umemwahidi atapata, bila ya kuja na sababu yoyote ile. Hakikisha bidhaa au huduma haziishi kabisa kiasi kwamba mteja anakuja na kukosa kile alichofuata. Fanya kila uwezalo kuhakikisha mteja anatoka kwenye biashara yako akiwa na alichofuata, na siyo sababu kwa nini hajapata. Hakuna sababu yoyote utakayompa mteja itamridhisha, hata kama atakubaliana na wewe.

Kama mteja hapati anachotaka kwenye biashara yako, atatafuta pengine ambapo anaweza kupata kile anachotaka. Hii ni njia rahisi kabisa ya kuwapoteza wateja wako, usikubali kuitumia kuua biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha