Huwezi kuwa na majibu ya kila kitu kwenye maisha, lakini unapaswa kuwa na majibu ya kila kitu kwenye biashara yako. Unapaswa kujua kila kitu kinachohusiana na biashara yako, kiasi kwamba unaweza kujibu chochote ambacho mteja anakuuliza. Na hiyo ndiyo kazi yako kama mfanyabiashara, kitu pekee kinachokutofautisha na wachuuzi.

Mteja anapofika kwenye biashara yako, au anapofanya mawasiliano na wewe, anahitaji kujua kila anachotaka kujua ni kwa namna gani biashara yako inamsaidia kupata anachotaka au kuondokana na changamoto alizonazo. Mteja atapata wasiwasi kama atataka kujua kitu kuhusu biashara yako, halafu wewe unakuwa huna uhakika, unaonekana kubabaika.

SOMA; VITU 100 AMBAVYO KILA MJASIRIAMALI ANATAKIWA KUJUA NA KUFANYA ILI KUFANIKISHA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.

Hebu chukulia mfano wewe unaumwa sana, umetoka na hofu kubwa na kwenda kwa daktari, unamweleza daktari matatizo yako, halafu daktari anakuambia sijui hata tufanye nini. Utajisikiaje kwenye hali kama hiyo?

Hivyo ndivyo mteja anapoisikia pale anapotaka kujua kitu kuhusu biashara yako, halafu wewe unakosa majibu. Ni wajibu wako kujua kila kitu kinachohusiana na biashara yako, na hakikisha kila mteja wako anaielewa vizuri biashara yako.

Unapaswa kuwa mtaalamu uliyebobea kwenye biashara unayofanya, tofauti na hapo wewe siyo mfanyabiashara, ni mchuuzi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha