Kama haupo makini na jinsi unavyoyaendesha maisha yako, utakuwa unajitengenezea majuto makubwa sana kwa baadaye. Majuto ambayo kinapofika kipindi unajutia, unakuwa huna tena la kufanya ili kubadili hali ilivyo kwa wakati huo.

Muuguzi Bronnie Warre kwenye kitabu chake cha majuto matano ya watu wanaokufa, kupitia kuwahoji watu waliokuwa wanakaribia kufa, anatuambia kitu cha kwanza ambacho wengi wanajutia ni kutokuishi maisha ambayo ni ya uhalisia kwao. Mwisho wa maisha ya watu, wanajutia kutokuishi maisha yao na badala yake kuishi maisha ambayo ni ya kuwafurahisha wengine.

Kitu kingine kinachoendana na hicho, ambacho utakijutia sana pale umri wako unapokuwa umeenda sana, ni kutokuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako. Kila mmoja wetu ana uwezo mkubwa sana ndani yake. Kila mmoja wetu anaweza kufanya zaidi ya anavyofanya sasa. Lakini usumbufu wa dunia na mazoea yamewafanya wengi kufanya chini kabisa ya uwezo wao.

Ni mpaka watu wanapofikia ukingoni mwa maisha yao, ndiyo wanagundua kwamba wangeweza kufanya zaidi, wanagundua kwamba walipoteza maisha yao kwa kufanya vitu ambavyo ni vidogo sana na havijawafanya waridhike na maisha yako.

SOMA; UKURASA WA 351; Majuto Kama Kichocheo….

Rafiki yangu, usisubiri mpaka maisha yafike ukingoni ndiyo ujutie hilo, wakati utakuwa huna cha kufanya. Leo hii, sasa hivi una cha kufanya. Una hatua ambazo unaweza kuchukua na ukayafanya maisha yako kuwa bora zaidi, ukaweza kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Kwa kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako, siyo tu kwamba utakusaidia wewe, bali itawasaidia na wengine pia.

Hivyo kila siku unapoamka, jiulize je kipi kikubwa unachoweza kufanya kwa siku hiyo? Kila unachoanza kufanya, jiulize je hicho ndiyo kikubwa na muhimu zaidi unachopaswa kufanya? Au kuna ambacho ni kikubwa na muhimu zaidi?

Usikubali kuendelea na maisha yako kwa mazoea, ishi maisha ambayo utaacha alama kubwa kwenye hii dunia. Na ni rahisi sana kama utajua uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kuufanyia kazi.

Usikubali usumbufu wa dunia ukufanye usahau uwezo mkubwa uliopo ndani yako, tumia uwezo huo kila siku na utaweza kupiga hatua kubwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha