Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WEKA KAZI…
WEKA KAZI ni kauli ambayo huwa napenda kukuambia mara kwa mara, na nitazidi kukuambia tena na tena na tena.
Kwa sababu, kwa tafiti zote zilizowahi kufanywa kuhusu mafanikio, kuna kitu kimoja ambacho kipo kwa kila anayefanikiwa.

Kitu hicho ni kazi, kazi hasa, na siyo kazi ya kitoto.
Kadiri unavyotaka kupata mafanikio makubwa, ndivyo kazi unayofanya inavyopaswa kuwa kubwa.
Na pale ulipo sasa, ni matokeo ya kazi uliyofanya huko nyuma.
Kazi unayofanya leo ndiyo inatengeneza kesho yako.

Mambo muhimu ya kukumbushana kwenye KUWEKA KAZI…
Unachotaka kiendane na kazi unayofanya, kwa maneno mengine usijidanganye ili kujifurahisha.
Usijiambie unataka kuwa bilionea halafu unafanya kazi masaa 10 pekee kwa siku na mwisho wa wiki hufanyi kazi. Utakuwa unajidanganya mwenyewe. Ubilionea utakutaka ufanye kazi mpaka masaa 18 kwa siku, siku 7 za wiki.

Usitafute sababu za kujieleza kwa nini hujaweka kazi. Weka kazi na matokeo yaonekane, na kama hakuna matokeo ya kuonesha, badala ya kupoteza muda kutafuta na kutoa sababu, tumia muda huo kuweka kazi.

Mwisho, fanya kazi unapokuwa unafanya kazi. Kile wengi wanaita kufanya kazi wala siyo kazi. Kufanya kazi huku unapokea simu na kujibu jumbe zisozohusiana na kazi, kufanya kazi huku kila baada ya muda mfupi unaperuzi mitandao ya kijamii, hapo hakuna kazi unafanya.
Unapofanya kazo, akili yako yote, mawazo yako yote, nguvu zako zote na imani yako yote inapaswa kuwa kwenye kazi hiyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuweka kazi hasa, kazi inayoendana na matokeo unayotaka. USIJIDANGANYE.

#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha