Tafiti nyingi zinaonesha kwamba watu ambao wana vipaji vikubwa kwenye maeneo fulani, huwa hawafanyi vizuri kama wale ambao hawana vipaji. Unakuta kuna watu wana kipaji kikubwa sana, lakini wanaofanya vizuri kwenye maeneo hayo ni wale ambao hawana vipaji.

Hii inaonesha kwamba, kwa wengi, kipaji ni kikwazo kwao kufanikiwa, badala ya kuwa kichocheo cha kufanikiwa. Na hili linaonekana wazi kwenye maisha ya wengi.

Utakuta watu wana kipaji kikubwa sana kwenye maeneo fulani ya maisha yao, lakini hakuna hatua kubwa wanazopiga. Ila wale wasio na kipaji, wanakuwa wamepiga hatua kubwa sana.

Kipaji kwa wengi kinageuka kuwa kikwazo kwa sababu mbalimbali;

Moja watu wanajiona kwa sababu wana kipaji basi hawahitaji kuweka kazi kubwa kama wengine. Na hapo watajisifu sana kwamba wala hawahitaji kufanya kazi sana, kazi kidogo tu kwao inaleta matokeo mazuri, kwa sababu wana kipaji. Na hapo ndipo wanaoweka kazi hasa wanapowaacha mbali.

Mbili ni jamii inayowazunguka wale wenye vipaji, inawafanya wajione ni wa pekee sana, kiasi kwamba hawahitaji kuteseka katika kuendeleza vipaji vyao. Kutokana na kusifiwa sana, wale wenye vipaji wanajiona kama wameshafanikiwa, kutoka tu kwenye sifa za wengine, na hivyo hawajitahidi sana.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Naked Millionaire (Muongozo Wa Uhakika Wa Kuelekea Kwenye Utajiri, Uhuru Na Utimilivu).

Rafiki, kipaji chochote ulichonacho, kinachangia mafanikio yako kwa asilimia 10 tu, asilimia 90 nyingine inatoka kwenye kazi, tena kazi hasa, siyo kazi ndogo, siyo kazi ya kitoto.

Hivyo acha mara moja kujidanganya na kipaji chako, acha kuificha ndani ya kipaji chako, unahitaji kuweka kazi kubwa sana kwenye chochote unachofanya hivyo jiandae na weka kazi sana.

Ukichukua kipaji ulicho nacho, kisha ukaweka kazi kubwa sana utapata matokeo makubwa sana. Unahitaji kuweka kazi kubwa kuliko hata wale wasiokuwa na kipaji wanayoweka. Hiyo ndiyo njia pekee ya kukuwezesha wewe kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha