Rafiki yangu mpendwa,

Nimekuwa nakuambia kwamba furaha ni zao la ndani yako mwenyewe. Kwamba furaha inaanzia ndani yako na siyo nje. Huwezi kununua furaha, bali unaweza kuikaribisha furaha kulingana na maisha unayoishi.

Watu wengi hufikiri wakifika umri fulani, wakimaliza kitu fulani au wakipata fedha na mali fulani. Ni mpaka wanapopata vitu hivyo ndipo wanajifunza kwamba vitu hivyo havileti furaha.

Kama ukiwa huna fedha huna furaha, basi jua pia ukiwa na fedha nyingi hutakuwa na furaha. Kama ukiwa peke yako huna furaha, basi jua hata ukiwa na mtu hutakuwa na furaha.

Na kwa kusisitiza, siyo kwamba ukifanikiwa utakuwa na furaha, bali ukiwa na furaha ndiyo utafanikiwa. Hivyo furaha yako ni hitaji muhimu sana la mafanikio yako.

Lakini kuna vitu ambavyo watu wamekuwa wanafanya, vitu ambavyo vinawaondolea furaha yao na kuwazuia kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia kitu kimoja cha kufanya ili uwe na furaha ya kudumu kwenye maisha yako. Kwa kufanya kitu hichi kimoja, utajiondoa kwenye tabia zinazokuzuia wewe usiwe na furaha.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Kitu kimoja muhimu unachopaswa kufanya ili uwe na furaha inayodumu ni KUJALI MAMBO YAKO. Wazungu wanasema MIND YOUR OWN BUSINESS.

Watu wengi, wanapoteza muda na nguvu nyingi za maisha yao kujali sana mambo ya wengine. Watu wanatumia muda na nguvu zao kutaka kujua nani kafanya nini na kwa nini, watu ambao hata hawawajui na hawana hata uhusiano nao wa karibu.

Watu wanatumia muda na nguvu kujadili maisha ya wengine, kujifanya wana ushauri mzuri sana wa jinsi gani watu hao wangefanya vizuri zaidi wakati watu hao hata hawawasikilizi.

Kufuatilia maisha ya wengine ni moja ya majukumu ya watu wavivu, watu wasiojua wapi wanaenda na maisha yao, watu wasiokuwa na ajenda binafsi na maisha yao na wasioweza kufanikiwa.

Kama upo kwenye kundi hili la kufuatilia maisha ya wengine, ondoka haraka kwa sababu siyo tu unapoteza muda na nguvu zako, bali pia unajizuia usiwe na furaha.

Kwa sababu tukiangalia kwa umakini, kila mtu anafanya mambo yake kulingana na akili zake zinavyomtuma. Sasa kama wewe unataka kuwa polisi wa dunia nzima, ambaye umejipa mamlaka ya kuwapangia watu wanapaswa kufanya nini na nini hawapaswi kufanya, unajitesa bure. Maana wale unaokuwa unawakosoa au kuwaambia kipi wanapaswa kufanya, hawakusikilizi na mbaya zaidi, hawajui hata kama upo hapa duniani.

Huu Ndiyo Uhuru Wako Wa Kweli Hapa Duniani Na Utakaokuwezesha Kufanikiwa.Huu Ndiyo Uhuru Wako Wa Kweli Hapa Duniani Na Utakaokuwezesha Kufanikiwa.

Ukuaji wa teknolojia, hasa mitandao ya kijamii, imechochea sana hali hii ya watu kufuatilia maisha ya wengine. Watu wanaweza kujua kila kinachoendelea kwenye maisha ya wengine kwa sababu muda wote wanawafuatilia kwenye mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii imefanya tabia hii ya kufuatilia maisha ya wengine kuwa kubwa na hatari zaidi.

Kwa sababu ni kwenye mitandao hii ya kijamii, mtu anaweza kumpangia mwingine awaze nini, aandike nini, aamini nini, aseme nini, asiseme nini na hata avae nini. Watu wamekuwa wanateseka na mitandao hii kiasi kwamba wamegeuka kuwa watumwa wa watu wengine.

Na sasa hivi, kila mwenye uwezo wa kuwa kwenye mtandao wa kijamii ni mchambuzi, mshauri na mkosoaji wa kila wanachofanya wengine. Watu wanapoteza muda na nguvu nyingi kwenye mitandao hii ya kijamii wakitaka kila mtu aishi kama wanavyotaka wao.

Rafiki yangu, ninachokuambia ni hichi, kama upo kwenye kundi hili la kufuatilia maisha ya wengine, ondoka haraka. Ondoa haraka pua yako kwenye maisha ya wengine na izamishe kwenye maisha yako. Kwa sababu nina uhakika pamoja na kwamba unajifanya unakosoa sana wengine, kuna mengi ambayo wewe mwenyewe yamekushinda.

Nina uhakika pamoja na kwamba unaweza kukosoa maamuzi ya kiongozi fulani, kuna vitu vingi kwenye maisha yako umeshindwa kuviongoza vizuri, huenda hata familia yako haipo vizuri kwa sababu ya maamuzi yako ya hovyo. Sasa hufikiri kwamba kama ungezamisha pua yako kwenye maisha yako, ukakazana kufanya maamuzi bora na familia yako ikawa vizuri, maisha yako hayatakuwa na furaha?

Kama muda unaotumia kukosoa wengine, kusema nani kakosea na nani kapatia, ungeutumia muda huo kujifunza zaidi kwenye kile unachofanya, unafikiri ungekuwa hapo ulipo sasa?

Kwa mfano kama ukaamua leo kutokutumia kabisa mtandao wowote wa kijamii, ukaifuta kabisa. Na kila siku ukatumia saa moja kujifunza kuhusiana na kazi au biashara unayofanya, unafikiri utabaki pale ulipo sasa?

Jali mambo yako rafiki yangu, hilo ndiyo jambo muhimu kwako, hicho ndiyo kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako. Waache wengine wajali mambo yao, na kama wapo watakaojipendekeza kujali mambo yao, waache maana wamechagua kupoteza muda na maisha yao wao wenyewe.

Anza leo kuweka kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako. Na kabla hujamkosoa au kumsema mwingine, angalia kwanza kama maisha yako yamekamilika kila eneo. Kama hayajakamilika, achana na kufuatilia maisha ya wengine na kazana na maisha yako.

Na kwa wale mnaojiambia kwamba lazima watu waseme, hatuwezi kuacha mambo yaende tu yanavyoenda, jua kabisa kusema kwako hakubadili chochote. Unajaza hewa tu na maneno yako, na unapoteza muda ambao ungeweza kuutumia kwenye mambo muhimu zaidi kwako. Pia waachie wasiojua wanaenda wapi wawe mapolisi wa dunia, wewe kazana kuwa polisi wako mwenyewe, ujisukume kufanikiwa zaidi.

SOMA; Huyu Ndiye ‘STAA’ Muhimu Unayepaswa Kumfuatilia Kila Siku Kwenye Maisha Yako Ili Ufanikiwe.

Mwanafalsafa mmoja amewahi kusema, chagua sumu yako na niache nichague sumu yangu mwenyewe. Akimaanisha kwamba, kila mtu kuna sumu anaichagua kwenye maisha yake. Wakati wewe unakazana kutoa ushauri kwa wengine, ukiamini unawasaidia sana, unajisahau kwamba kuna ushauri ambao ungeuhitaji sana, lakini kwa sababu hujifuatilii kama unavyowafuatilia wengine, unajiua kwa sumu yako mwenyewe, huku ukikazana kuondoa sumu kwa wengine.

Jali mambo yako rafiki yangu, hicho ndiyo kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako. Vingine vyote havina umuhimu kama hujajali mambo yako. Na huu siyo ubinafsi, bali ni njia bora kabisa ya kuweza kuwasaidia wengine kuwa na maisha bora sana kwao.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha