Usemi unaopaswa kuukumbuka kwenye biashara yako kila siku ni huu, mara zote mteja yupo sahihi. Hata kama kwa upande wako anakosea, jua kwamba kwa upande wake na kwa mtazamo wake, mteja mara zote yupo sahihi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya kosa sana kujaribu kuwaonesha wateja hawapo sahihi, kinachotokea wateja wanajisikia vibaya na wanaamua wasinunue kabisa.

Kwa upande wa bei, jua kabisa kwamba mteja atakaposikia bei yako kwa mara ya kwanza, atakuambia bei yako iko juu. Sasa badala ya kuanza kubishana naye kwamba bei yako haipo juu, itakuwa vyema kama utaanza kwa kukubaliana naye, kisha ukamuuliza swali moja muhimu sana.

SOMA; BIASHARA LEO; Jinsi Ya Kumjibu Mteja Anayekuambia Wengine Wanauza Kwa Bei Ndogo Kuliko Wewe…

Mwulize mteja anasema bei yako iko juu kwa kulinganisha na nini? Ni kipimo gani anatumia kupima bei mpaka akasema ipo juu?

Na hapo sikiliza jibu la mteja, na tumia jibu lake kumfanya aone bei anayolipa ipo juu na atanufaika zaidi kwa kulipa bei hiyo.

Mfano mteja amekujibu bei yako iko juu ukilinganisha na wafanyabiashara wengine wanaouza unachouza. Kubaliana naye, huku ukijua kabisa bei ya wengine ni kiasi gani, ila pia mweleze huduma za ziada atakazopata kwa kununua kwako badala ya kununua kwa mwingine.

Mteja anakujibu bei iko juu kulingana na bajeti yake, angalia ni huduma au bidhaa gani nyingine unayo ambayo itamfaa kwa bajeti yake, au mshauri njia bora ya kulipia ili kuendana na bajeti yake.

Ukijipa muda wa kujua sababu ya mteja kusema bei ipo juu, utaona ni jinsi gani hampishani sana, na utaweza kumuuzia mteja wako kitu ambacho atanufaika nacho sana.

Kumbuka, jukumu lako la kwanza kwenye biashara ni kutengeneza wateja wanaoiamini na kuitegemea biashara. Na utafanya hivyo kama utawasikiliza wateja na kuchukua hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha