Kabla hujakimbilia kupunguza bei kwenye biashara yako kwa sababu wengine wanapunguza bei, kuna hatua nyingi unazoweza kuchukua na zikaongeza thamani sana kiasi kwamba bei yako inaonekana si kitu kulingana na mteja anachopata.

Moja ya vitu unavyoweza kufanya ni kuyamiliki matatizo ya wateja wako. Yale matatizo ambayo biashara yako inatatua. Mfanye mteja akija kwako, aone kama anatua mzigo mzito uliokuwa unamtesa na wewe unaufanyia kazi kwa niaba yake.

Hichi ni kitu kimoja ambao wanauza kwa bei rahisi hawawezi kufanya, kwa sababu hawawezi kumudu kumiliki matatizo ya wateja wao kwa faida ndogo wanayopata.

Wewe unapokuja na mbinu hii, unawafanya wateja wakutegemee wewe na hivyo wawe tayari kulipia gharama unazotoza, ambazo ni za juu ukilinganisha na wengine wanavyotoza.

Pia kwa kubaki na bei ya juu huku ukitoa huduma bora, unawavutia wateja ambao ni bora kwako. Na wale wanaoangalia bei tu unawaacha waende kuwatesa washindani wako wa kibiashara. Kwa sababu hakuna wateja wanaotesa kama wale wanaotaka kununua kitu kwa bei rahisi.

Miliki matatizo ya wateja wako, wafanye wateja wakutegemee wewe kwenye lile tatizo unalowatatulia na watakuwa wateja waaminifu kwako wasioona bei yako kama ni kubwa, licha ya kwamba ipo juu kuliko ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha