Rafiki yangu mpendwa,

Tayari tumemaliza juma jingine la mwaka huu 2018, tumemaliza juma namba 31 ambalo naamini kama unasoma hapa, lilikuwa juma bora sana kwako. Najua kwa sababu kama umekuwa unafanyia kazi yale ninayokushirikisha kila siku, basi utakuwa unapiga hatua kubwa. Hata kama hupati unachotaka, basi unajifunza njia bora zaidi za kupata unachotaka.

Karibu kwenye tano za juma, ambapo nakuandalia mambo matano muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi kwenye juma jipya unalokwenda kuanza ili uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu.

Kanuni yetu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MATOKEO MAKUBWA. Unahitaji kufanya vitu viwili vitu, kupata maarifa sahihi na kuchukua hatua kubwa kulingana na maarifa uliyopata na hapo utaweza kupata matokeo makubwa sana. Kuwa na maarifa bila kuchukua hatua ni uvivu, na kuchukua hatua bila ya maarifa ni kupoteza muda na nguvu zako. Weka hivyo viwili pamoja na utapiga hatua kubwa.

Rafiki yangu, yafuatayo ni matano muhimu niliyokuandalia, jifunze, yatafakari kwenye maisha yako kisha chukua hatua ili juma unalokwenda kuanza liwe bora sana kwako.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUJUA UKWELI KWENYE MAFURIKO YA TAARIFA.

Tunaishi kwenye zama za taarifa, zama ambazo wale wenye taarifa sahihi na wanaochukua hatua ndiyo wanaofanikiwa sana. Katika zama hizi, kwa siku moja tu zinazalishwa taarifa nyingi kuliko taarifa zilizokuwa zinazalishwa mwaka mzima kwenye karne ya 15.

Pamoja na wingi huu wa taarifa, kuna changamoto kubwa ambayo tunakutana nayo, changamoto hiyo ni usahihi wa taarifa tunazopata. Mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii imerahisisha sana usambaaji wa taarifa. Hivyo mtu yeyote anaweza kusema chochote kwa namna anavyotaka yeye.

Ukuaji huu wa teknolojia umewafanya baadhi ya watu kusambaza taarifa wanazotaka kwa manufaa yao, ambazo siyo sahihi na siyo kweli. Tumekuwa tunaona jinsi baadhi ya taarifa zisizo sahihi zinavyosambaa kwa kasi na kuleta madhara makubwa kwa wengi.

Katika wakati kama huu, tunahitaji kuwa na msingi sahihi wa kujua taarifa yoyote tunayoipokea kabla ya kuchukua hatua.

Waandishi Bill Kovach na Tom Rosenstiel wanatushirikisha jinsi ya kutambua usahihi wa taarifa tunazopata kupitia kitabu chao cha BLUR; HOW TO KNOW WHAT’S TRUE IN THE AGE OF INFORMATION OVERLOAD.

Waandishi wanaanza kwa kutuonesha jinsi gani miongo mitatu iliyopita, kabla ya kuja kwa intaneti, taarifa zilivyokuwa zinadhibitiwa na kuhakikiwa usahihi wake. Kulikuwa na vyombo vichache vya habari na waandishi wa habari walikuwa wanafanya kazi yao kwa weledi mkubwa, wakijua ni jukumu lao kuwapa watu taarifa sahihi.

Lakini kwa zama hizi, kila mtu ni mwandishi wa habari, na hata wale ambao kazi yao ni uandishi wa habari, wanasukumwa zaidi na umaarufu wa taarifa kuliko ukweli wake. Wengi wanakimbia kutoa taarifa siyo kwa sababu ni sahihi, ila kwa sababu ndiyo taarifa maarufu au ndiyo kitu ambacho watu wanataka.

Hali hii imesababisha taarifa zisizo sahihi na zisizo za kweli kusambaa kwa kasi, hasa pale watu wanapojua kile wengi wanapenda, wanawapa hicho.

Waandishi wanatuambia, kwa sasa nguvu ya kuchagua taarifa na kupima usahihi wake imeondoka kwa waandishi, na haipo kwa serikali, bali imekuja kwa mwananchi mmoja mmoja. Wewe kama mlaji wa taarifa mbalimbali, ndiye unapaswa kujali kama taarifa ni sahihi kwako na kuifanyia kazi au siyo sahihi na kuachana nayo.

MAPINDUZI NANE KWENYE USAMBAAJI WA TAARIFA.

Katika historia ya kustaarabika kwa binadamu, kumekuwepo na mapinduzi nane kwenye usambaaji wa taarifa. Hichi tunachoona sasa, kilishatokea mara nyingi huko nyuma. Kila mapinduzi yamekuwa bora kuliko awali, na yamekuwa yanaleta nafasi ya taarifa zisizo sahihi kusambaa.

Mapinduzi ya kwanza yalikuwa kusambaza taarifa kwa michoro ya mapangoni. Haya ni mapinduzi yaliyoanza miaka 15,000 kabla ya kuja kristo. Hii ilikuwa njia kuu ya kufundishana na kupeana taarifa.

Mapinduzi ya pili yalikuwa hadithi na mazungumzo ya mdomo. Hapa taarifa ziliuwa zikisambaa kwa hadithi ambazo watu walikuwa akiambiana. Mapinduzi haya yalikuwa miaka 5000 kabla ya kristo.

Mapinduzi ya tatu yalikuwa kusambaza taarifa kwa maandishi. Haya yalikuwa mapinduzi makubwa kwani maandishi yaliweza kudumu kwa muda mrefu na usahihi wake kutokubadilika kama kwenye hadithi.

Mapinduzi ya nne uchapaji wa maneno. Mapinduzi ya tatu yalikuwa maandishi ya maneno kwa mkono, mapinduzi ya nne yakaja na uchapaji wa habari. Hili lilichochea sana upatikanaji wa taarifa kwa usahihi. Kabla ya kuwepo kwa mfumo wa uchapaji, mtu mmoja alikuwa anaandika biblia nzima kwa mkono kwa mwaka mzima. Lakini uchapaji ulirahisisha upatikanaji wa vitabu kama biblia na ndipo watu wengi walipoweza kusoma na kupata ukweli kuliko kuambiwa kile ambacho watu wanachagua kuwaambia.

Mapinduzi ya tano ni simu ya upepo. Mapinduzi ya uchapaji yalirahisisha uzalishaji wa maarifa, lakini usambazaji haukuwa wa kasi kubwa. Kutoka kupata taarifa, mpaka kuchapa ilichukua muda. Na hapa ndipo simu ya upepo ilipoleta mapinduzi, ambapo usambaaji wa taarifa ulikuwa wa haraka kuliko kwenye uchapaji pekee.

Mapinduzi ya sita ni redio. Ujio wa redio uliwezesha watu kusikia kile kinachoendelea moja kwa moja. Hakukuwa tena na haja ya kusubiri mpaka habari ichapwe, watu walisomewa moja kwa moja.

Mapinduzi ya saba ni televisheni, hapa sasa watu waliweza kuona kila ambacho kinatokea, na siyo tu kusoma na kusikiliza.

Mapinduzi ya nane ni haya tunayoishi sasa, taarifa za kidigitali kwenye zama hizi za intaneti na mitandao ya kijamii. Katika zama hizi, kila mtu ni mzalishaji na mlaji wa taarifa.

Kwenye mapinduzi ya nyuma, ilikuwa rahisi kwa watu wachache kudhibiti taarifa gani watu wapate. Mfano uongozi wa nchi uliweza kuzuia  habari gani zisisambae kwa magazeti, tv au redio, pia uliweza kuzuia aina fulani ya vitabu visichapwe au kusambazwa. Hii ilikuwa nzuri pale habari zinapokuwa siyo nzuri, lakini pia ilikuwa mbaya pale uongozi unapotaka kusambaza propaganda zake wenyewe. Mfano ukiangalia serikali zote za kidikteta ambazo zimewahi kuwepo, vyombo vya habari vimekuwa vinatumika sana kusambaza propaganda fulani, kiasi cha wananchi kuamini kile wanachoambiwa ndiyo ukweli.

Lakini kwenye zama tunazoishi sasa, hakuna tena mwenye uwezo wa kumiliki taarifa au kuzuia watu wasipate taarifa fulani. Kwa sababu kila mtu anayo nguvu ya kusambaza na kupokea taarifa yoyote. Japo hili linakuwa faida kwa walaji wa taarifa, lakini pia linakuja na hatari moja, ni vigumu sana kujua usahihi wa taarifa unazopata hasa kwenye mtandao. Watu wengi wamefanya maamuzi kwa taarifa zisizo sahihi kitu ambacho kimewagharimu sana.

Waandishi wa kitabu cha BLUR, wametupa msingi mzuri sana wa kujua usahihi wa taarifa yoyote tunayoipokea. Tukiweza kutumia msingi huu, tutaweza kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia taarifa sahihi pekee.

MASWALI SITA YA KUULIZA ILI KUJUA USAHIHI WA TAARIFA UNAYOPOKEA.

Njia pekee ya kupata usahihi wa taarifa yoyote unayopokea, waandishi wa kitabu wanatuambia ni kuwa na wasiwasi na kila taarifa unayoipata. Usichukulie vitu kirahisi na hoji kila kitu. Jifanye hujui chochote na taka kujua ukweli.

Na hapa kuna maswali sita ya kuuliza na kujiuliza ili kujua usahihi wa taarifa yoyote unayopokea.

Moja; je ni aina gani ya taarifa unapokea? Taarifa zote unazopokea hazifanani. Unaweza kuwa unapokea taarifa ya tangazo, taarifa ya propaganda, au taarifa ya udaku. Unahitaji kujua aina ya taarifa unayopokea ili kutafuta usahihi wake.

Mbili; je taarifa imekamilika? Na kama hapana, kipi kinakosekana? Ukishajua aina ya taarifa unayopata, jiulize kama taarifa hiyo imekamilika. Kama kila ulichopaswa kujua kwenye taarifa hiyo kipo. Kama taarifa haijakamilika, jua nini kinachokosekana. Taarifa zisizo sahihi huwa zinaacha baadhi ya vitu kwa makusudi ili watu wasiweze kuona makosa ya taarifa hiyo yako wapi.

Tatu; je chanzo cha taarifa hiyo ni nani au nini? Na kwa nini uamini chanzo hicho cha taarifa? Kama kuna gazeti la simba na gazeti la yanga, unafikiri habari zitakuwa sawa kwenye magazeti hayo? Jibu ni hapana, gazeti la simba litainadika vizuri simba kuliko yanga, kadhalika kwenye gazeti la yanga. Unapopata taarifa, jiulize chanzo cha taarifa ni nini na chanzo hicho kinanufaikaje na taarifa hiyo. Hapa ni sehemu nzuri sana ya kujua propaganda.

Nne; je ni ushahidi gani unatolewa na taarifa hiyo na umepimwa na kuchaguliwaje? Chochote unachokipata kwenye taarifa, lazima ujue ni kwa namna gani kimepimwa na kudhibitishwa kuwa sahihi. Au wale waliochagua upate habari hiyo walitumia vigezo gani mpaka kuileta habari hiyo kwako?

Tano; je ni maelezo gani yanaweza kuwa mbadala wa taarifa unayopata? Kabla hujakubaliana na taarifa unayopata, jiulize kama kinyume chake inaweza kuwa sahihi. Yaani kama taarifa inakuambia hiki ni kitu cheupe, jiulize kama kinaweza kuwa kitu cheusi kisha angalia ushahidi unaoweza kusapoti kile unachofikiria wewe. Mara nyingi sana unaweza kuona makosa ya taarifa pale unapofikiria kinyume chake na kukuta kumbe kinyume chake ndiyo sahihi zaidi.

Sita; je unajifunza kile ulichotaka kujifunza? Hili ndiyo swali muhimu na la mwisho, ambapo hata kama taarifa ni sahihi, je ni sahihi kwako? Je inakusaidia wewe kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yako?

Haya ndiyo maswali sita muhimu sana ya kujiuliza na kujipa majibu kwa taarifa yoyote unayopokea kwenye zama hizi za mafuriko ya taarifa. Huhitaji kufanya hivi kwa kila taarifa, maana nyingi utazipuuza moja kwa moja. Lakini pale unapokutana na taarifa ambayo inakuhitaji ufanye maamuzi yatakayobadili kabisa maisha yako, au yanayokugharimu muda, fedha na nguvu, basi itakuwa vyema ukitumia muda wako kujiuliza na kujipa majibu ya maswali hayo sita.

Vinginevyo pata muda usome kitabu hichi kwa ukamili wake, utajifunza mengi mno. Lakini kama hutapata muda wa kusoma kitabu kizima, basi shika sana maswali haya na yafanyie kazi wakati wote unapohitaji kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

#2 MAKALA YA WIKI; DALILI TANO ZA KUANGALIA KWENYE FURSA ILI USITAPELIWE.

Juma lililopita kuna ndugu yangu wa karibu sana alikuwa ananitafuta, akiniambia ana shida sana ya kuonana na mimi. Basi nilimpa nafasi na tukakutana. Akaniambia kuna fursa nzuri sana ameipata, ambapo amekwama kiasi kidogo sana cha fedha. Kama nitamsaidia kiasi hicho, basi ndani ya miezi miwili mpaka mitatu atanirudishia kiasi hicho bila ya shida yoyote. Nilipata shauku ya kujua zaidi ni fursa gani hiyo aliyoipata. Basi akanza kunieleza.

Alichonieleza ni hichi, alikuwa amekutana na watu wakamwambia kwamba wao wanafanya kilimo cha matikiti maji. Na wakamwambia wanaweza kumsaidia na akaweza kulima na kufanikiwa. Walimwambia kwamba, kwa heka moja ya matikiti maji, ataweza kupata mavuno ya thamani ya milioni kumi na mbili. Hivyo anahitaji kuwekeza kama milioni tatu tu na kazi zote zitafanywa bila ya yeye kuhusika sana. Lakini mavuno yatakuwa mazuri na atapata milioni zake 12.

Ni fursa kubwa sana, uweke milioni tatu na baada ya miezi miwili mpaka mitatu upate milioni 9 za ziada, yaani mara tatu ya ulichowekeza. Ndugu yangu huyu hakuweza kutulia, alipambana sana apate kiasi hicho cha milioni tatu, na alikuwa tayari ana akiba yake ya milioni mbili.

Hapa ndipo nilikaa naye chini na kumweleza ukweli halisi anaopaswa kujua kabla hajaingia kwenye kilimo. Nilimwelekeza vizuri sana kwamba mafanikio yapo, lakini siyo hayo anayoambiwa, na nilimweleza kwamba ataanguka vibaya, kwa sababu alikuwa na mategemeo makubwa sana.

Nilistuka sana kuona kumbe bado watu wanadanganyika kirahisi hivyo. Hivyo nilikaa chini na kuandika makala, yenye dalili tano unazopaswa kuziangalia kwenye fursa unayoshirikisha. Ukiziona tu dalili hizo tano, kimbia haraka sana, kwa sababu ukisubiri kidogo tu unalizwa.

Unaweza kuisoma makala hiyo ya wiki (na acha chochote unachofanya uisome sasa, maana itakusaidia sana) hapa; Ukiona Dalili Hizi Tano Kwenye Fursa Yoyote Unayoambiwa, Kimbia Haraka, Hakuna Fursa Hapo Bali Utapeli. (https://amkamtanzania.com/2018/08/04/ukiona-dalili-hizi-tano-kwenye-fursa-yoyote-unayoambiwa-kimbia-haraka-hakuna-fursa-hapo-bali-utapeli/)

#3 TUONGEE PESA; KILA MTU APENDE PESA ZAKE MWENYEWE.

Kuna kosa moja naliona kwa wengi inapokuja swala la fedha. Watu wanafikiri kuna mtu anajali kuhusu fedha zao kuliko wao wenyewe. Hivyo mtu anafungua biashara na kuacha wale wanaomsaidia kwenye biashara hiyo wafanye kile wanachojisikia kufanya.

Wengine wanaambiwa watoe fedha zao kwa wengine ambao watazifanyia kazi halafu wao watavuna faida tu.

Ninachokuambia rafiki, penda fedha zako mwenyewe. Kila mtu apende fedha zake mwenyewe. Na kama hutazipenda na kusimamia fedha zako, hakuna atakayefanya hivyo kwa ajili yako.

Popote unapoweka fedha zako, hakikisha una udhibiti wa kutosha, unajua kila kinachoendelea na jinsi fedha hiyo inavyofanya kazi. Usitake njia za mkato, ambazo watu wanakuambia wanazalisha fedha zako sijui kwa kuotesha mbegu au kufanya nini.

Na kama umeanzisha biashara na una watu wanakusaidia kwa sababu huna muda mwingi wa kuwa kwenye biashara hiyo, basi penda sana fedha zako kiasi cha kutaka kujua kila wakati fedha ya biashara iko wapi. Mkipiga mahesabu halafu kukawa na elfu moja haijulikani iko wapi, haipo kwenye mali wala haipo kwenye fedha keshi, lazima hiyo elfu moja itafutwe mpaka ijulikane iko wapi.

Wengi huwa wanasema elfu moja kitu gani, itakuwa mahali tu, tusipoteze muda kwa elfu moja. Ambacho hawajui ni kwamba baada ya muda inaacha kuwa elfu moja na inakuwa elfu 5, baadaye elfu 10, baadaye laki, mwishoni mtaji wa biashara unazidi kupungua na biashara inakufa.

Ipende sana pesa yako kiasi kwamba mtu anapojua anahusika na fedha yako, awe makini mno, maana anajua huachii hata mia isionekane imeenda wapi. Usipopenda fedha zako mwenyewe, wenzako watakusaidia kuzipenda, na hutakaa nazo muda mrefu.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; USIKOSE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Rafiki yangu mpendwa, nimeshakupa taarifa za SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, tukio kubwa sana la kimafanikio linalotokea mara moja tu kwa mwaka, na mwaka huu 2018 linatokea tarehe 03/11/2018. Usipange kitu kingine chochote kwenye tarehe hiyo, na kama utahitaji kusafiri kuja Dar kwenye tukio hili, basi ratiba yako kuanzia tarehe 02/11 mpaka tarehe 04/11 isiwe na kitu kingine chochote, bali SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Semina itafanyika Dar es salaam na ada ya kushiriki semina hii, ambayo itahusisha huduma zote za siku ya semina ni shilingi 100,000/=. Mwisho wa kulipa ada hii ya kushiriki ni tarehe 31/10/2018. Na pia unaweza kulipa kidogo kidogo kadiri unavyoweza wewe. Kuanzia elfu moja kwa siku, elfu 10 kwa wiki au elfu 30 kwa mwezi. Nitapokea na kuweka kumbukumbu zako ili usikose semina hii muhimu sana kwako.

Ili kuhakikisha unaendelea kupata taarifa za semina hii, nimeandaa kundi maalumu la wasap kuhusu semina. Naomba kama tu utashiriki semina hii basi ujiunge. Kama unajua hutashiriki usijiunge, ili wale wanaoshiriki wapate nafasi. Kujiunga na kundi hili, bonyeza kiungo hichi hapa; https://chat.whatsapp.com/L3F4jaeYcZO4drSCxWYrPr

Karibu sana kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, tushirikishane yale muhimu sana kwenye safari yetu ya mafanikio.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HUOGOPI KUFA BALI UNAOGOPA KUISHI.

Death is not the biggest fear we have; our biggest fear is taking the risk to be alive — the risk to be alive and express what we really are. – Don Miguel Ruiz

Nani asiyejua kwamba siku moja atakufa? Tunaona watu wanakufa kila siku, na tunajua siku moja itakuwa sisi ndiyo tunaagwa. Hivyo wanachohofia wengi kwenye maisha yao siyo kifo, bali watu wanahofia kuishi. Ndiyo, kinachokuogopesha wewe siyo kifo, bali kuishi maisha ya kweli kwako, maisha yenye maana kwako. Kwa sababu kuishi maisha yako kunakutaka uchukue hatua ambazo zinaweza kuwa hatari na ukashindwa, na hutaki wengine waone umeshindwa. Hivyo unaishi maisha yako yote ukiogopa kuishi maisha yako, ni aina gani ya maisha hiyo?

Ondoka kwenye hiyo hofu ya kuishi maisha yako na anza sasa kuishi maisha halisi kwako, maisha ya kweli kwako, maisha yenye maana kwako.

Rafiki, haya ndiyo matano muhimu nakushirikisha ujifunze na uweke mikakati ya kuyafanyia kazi kwenye maisha yako, ili uweze kufikia mafanikio makubwa sana. Nakutakia kila la kheri kwenye juma namba 32 tunalokwenda kuanza. Likawe juma la kupata taarifa sahihi, kuepuka kutapeliwa, kuzipenda fedha zako, kujiandaa na semina na pia kuondokana na hofu ya kuishi maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji