Kuna tukio la kisaikolojia linatokea pale mteja anapotoa fedha yake aliyoipata kwa shida kukulipa kwa kile unachouza. Kwa sababu kwanza akishakupa fedha hiyo maana yake hawezi kuitumia kwa mambo mengine ambayo yanaweza kuwa muhimu kwake.

Na pili, mteja anahitaji kupata uhakika kwamba anacholipia ni sahihi na moja ya kipimo anachotumia ni ugumu wa kupata kitu.

Upo mfano mmoja kwamba mtu alienda kwa daktari wa meno akamuuliza ni shilingi ngapi kung’oa jino, daktari akamjibu shilingi elfu 30. Akamuuliza itachukua muda gani kung’oa jino hilo, daktari akamjibu dakika 5. Mtu yule akastuka, yaani dakika tano tu ndiyo uchukue elfu 30? Daktari akamjibu kama shida yako ni muda naweza kung’oa jino hilo hata kwa saa nzima.

Mfano huu unatuonesha jinsi gani watu wanategemea kupata kwa kiasi wanacholipa.

Na kama wanavyosema, dawa inayofanya kazi ni ile inayouma. Na wapo watu ambao kama anaumwa na hakuchomwa sindano, anaamini hajatibiwa na kweli hatapona. Lakini kama atachomwa sindano, hata kama ni ya maji, basi imani yake inamponesha.

Unahitaji kujumuisha hili kwenye biashara yako, hasa pale unapompa mteja bei. Mfanye mteja ajue ni thamani gani hasa anayopata kwa anacholipia. Aache tu kuangalia kile ambacho anaona kwa haraka na ajue kwa ndani ni thamani ipi halisi anayolipia.

Wakati mwingine, unahitaji kuongeza thamani zaidi kisaikolojia, kwa kufanya unachotoa kuwa kigumu kupatikana kiasi kwamba mteja akikipata, anakuwa tayari kulipia kwa sababu anajua hawezi kupata tena.

Kadiri unavyoielewa biashara yako na kuwaelewa wateja wako, ndivyo unavyoweza kuongeza thamani ya kisaikolojia kwa wateja wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha