Tunaishi kwenye dunia ambayo watu wanajali zaidi mwonekano wa nje kuliko matokeo ambayo wanatoa.

Watu wanapenda kuonekana wamefanikiwa wakati matokeo wanayopata siyo ya mafanikio.

Watu wanapenda kuonekana wanajua wakati wanachojua hakiwasaidii kuwa bora.

Watu wanapenda kuonekana wana furaha muda wote wakati maisha yao hayaakisi aina hiyo ya furaha.

Nilichojifunza kupitia wengi ni kwamba, unaweza kuweka nguvu zako kwenye mwonekano, ukawa kama mtu anayeigiza. Au ukaweka nguvu zako kwenye kupata yale matokeo unayotaka.

Na uchaguzi ni wako, kama unalipwa ili kuigiza basi endelea kuigiza. Lakini kama hakuna anayekulipa, unaigiza tu ili wengine wakuone, nakuambia unapoteza muda, maana hakuna hata anayekuona, maana wengine nao wako bize kuigiza.

SOMA; UKURASA WA 956; Usijioneshe, Bali Onekana…

Dunia imejaa sana waigizaji, na ukiwa mwigizaji, jua unavutia waigizaji kwenye maisha yako.

Ondoka kwenye kundi la kuigiza, ondoka kwenye kundi la kuonekana na nenda kwenye kundi la kuzalisha, kundi la kufanya, kundi la kutoa matokeo bora zaidi wakati wote.

Na hata kama hakuna anayeona au kukubali kile unachozalisha, wewe unaona, na kama unazalisha kwa viwango unavyotaka, wewe unaridhika, na ukisharidhika unawavutia wale sahihi wanaotumia matokeo yako na siyo wale wanaoangalia kile cha nje.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha