Kama kuna kitu kilipaswa kuwa rahisi kwenye maisha yetu, ni mtu kuwa wewe, kuwa kile ambacho umezaliwa na kuletwa hapa duniani kuwa. Kama ambavyo ukichukua yai la kuku na ukatamishia kwenye kanga, bado atatoka kuku, na hata kifaranga wa kuku atalelewa pamoja na vifaranga wa kanga, bado atabaki kuwa kuku.
Lakini kwa sisi binadamu hilo linakuwa gumu sana, ni rahisi kuwa kama wengine walivyo kuliko kuwa wewe binafsi, kuwa kile ambacho unapaswa kuwa.
Na sababu pekee inayofanya kuwa wewe kuwe kugumu ni kwamba kila mtu anataka kukuweka wewe kwenye kundi fulani, ili aweze kukutumia, aweze kukutawala na aweze kupata chochote anachotaka kutoka kwako.
Na hili lilianzia kwenye familia, haikuwa rahisi wewe kufanya kila ulichotaka, kwa sababu wazazi wako wasingeweza kukupa kila ulichotaka, hivyo uliambiwa unapaswa kuwa kama watoto wengine, ukabeba hilo.
Ulipoenda shule nako, ulipojaribu kufanya vitu vingine ambavyo ni muhimu zaidi kwako uliambiwa uache na ukazane na masomo kama wengine ili ufaulu.
Ukirudi kwenye jamii, wanaotangaza biashara zao wanakuambia watu kama wewe wanafanya vitu kama hivi, hivyo unajikuta unafanya vitu fulani kwa sababu umeambiwa kila mtu ndiyo anafanya.
Ukienda kwenye ajira nako mwajiri anakuambia nini unapaswa kufanya .
Na hata kwenye maisha ya kawaida, serikali ya nchi yako inataka uwe kwenye kundi fulani ili utawalike vizuri.
Kwa mazingira haya, unaweza kuona ni kwa jinsi gani kuwa wewe ni kugumu. Pamoja na kuwa ni wimbo unaorudiwa sana kwa wale wanaotaka kufanikiwa, siyo rahisi kuwa wewe kama inavyosemwa.
Ili kuwa wewe unahitaji kuvuka nguvu kubwa sana inayojaribu kukuweka kwenye makundi mbalimbali. Unahitaji kuwa tayari kuvuka changamoto na vikwazo vingi vitakavyowekwa mbele yako na wale wanaotaka uwe kwenye namna fulani.
Lazima ujitoe sana ili kuweza kuwa wewe, na pia uwe tayari kushindwa na kuamka tena ili uweze kuwa wewe kweli.
Kuwa wewe ni kugumu sana kwenye dunia ambayo kila mtu anataka kuwa kama wengine. Pia itakutaka ufanye vitu ambavyo wengine hawawezi kukuelewa na hapo ndipo upinzani unapoanzia.
Jua nini unataka kuwa na chagua kuwa kitu hicho, usikubali kwa namna yoyote ile, mtu yeyote au kitu chochote kikuzuie kuwa kile unachotaka kuwa. Hayo ndiyo maisha halisi kwako, mengine tofauti na hayo ni maigizo na hayawezi kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,