Rafiki yangu mpendwa,

Waswahili wanasema subira yavuta heri, kwamba yeyote mwenye uwezo wa kusubiri basi atapata kile kilicho bora. Lakini kwa maisha tunayoishi zama hizi, subira imekuwa kitu adimu sana.

Kila mtu anataka kitu na anakitaka sasa. Asipokipata atatafuta kila aina ya njia ya mkato ya kupata, na pale njia hizo zinaposhindwa basi anaishia kulalamika au kuwalaumu wengine kama chanzo cha yeye kukosa anachotaka.

Watu wamekuwa wanasukumwa na tamaa ya kupata vitu haraka na kwa urahisi kiasi cha kusahau misingi muhimu ya kupata chochote unachotaka. Misingi ambayo ni kazi, kutoa thamani na kuwa na subira.

Pia watu wengi wamekuwa na uraibu (ulevi) kwenye vitu ambavyo havina msaada kwao. Watu wengi wamekuwa walevi wa habari, mitandao ya kijamii, kufuatilia maisha ya wengine kiasi kwamba wameyasahau kabisa maisha yao.

vitabu softcopy

Leo nakwenda kukushirikisha hatua muhimu za kuchukua ili kuishinda tamaa, kuondokana na uraibu na kuweza kujijengea uraibu kwenye maisha yako.

Karibu tujifunze, uweze kuchukua hatua na maisha yako yawe bora zaidi.

  1. Jua ni tamaa zipi zinazokuangusha, ulevi upi unakutesa na wapi unakosa subira.

Hatua ya kwanza kwenye kutatua tatizo lolote ulilonalo ni kujua tatizo hasa ni nini. Kwa sababu usipojua tatizo, chochote utakachofanya kitaongeza zaidi tatizo badala ya kutatua.

Jijue upo wapi kwenye maeneo haya matatu;

Jua ni tamaa zipi ambazo zimekuwa zinakushinda kila mara. Chochote ambacho unajua siyo sahihi kwako kufanya, lakini mara kwa mara unajikuta unakifanya, na hilo limekuwa halikupendezi.

Jua pia ni ulevi gani ambao tayari umeshajijengea kwenye maisha yako. Angalia ni mambo gani ambayo hayana mchango wowote kwenye mafanikio makubwa unayotaka, lakini unajiambia huwezi kuacha kufanya, au unakazana kuacha lakini unashindwa.

Na pia jua ni maeneo gani ya maisha yako ambayo umekosa subira. Jua ni vitu gani umekuwa unaharakisha kufanya na ukaishia kupata matokeo ambayo siyo mazuri.

  1. Angalia nini kimefanya uwe hapo ulipo.

Popote ulipo sasa, haupo tu kwa bahati mbaya, kuna vitu vimekufanya uwe hapo na kuna vitu vinaendelea kukuweka hapo.

Tamaa ulizonazo huenda ni kwa sababu unafikiri kwenye uhaba, au unafikiri unapaswa kupata kila unachotaka kwa sababu hakuna namna ya kupata kingine bora.

Ulevi ulionao inaweza kuwa ni njia ya wewe kutoroka kufanya yale muhimu. Pia wale wanaokuzunguka wanaweza kuwa sababu ya wewe kuendelea kuwa kwenye ulevi huo.

Kukosa kwako subira kunaweza kuwa kumetokana na uongo uliolishwa na wale waliokuzunguka. Pale vitu visivyo sahihi vinapotukuzwa kuliko vitu sahihi. Kama unatumia muda mwingi kupata taarifa za wanaoshinda bahati nasibu, utajiambia huhitaji kufanya kazi na kusubiri ndiyo ufanikiwe, ukiwa na bahati tu na kushinda unafanikiwa.

  1. Funga

Hatua nzuri ya kuimarisha uwezo wako wa kuwa na subira na hata kufanya maamuzi ni kufunga. Kufunga kutakusaidia sana kuwa na subira na hata kuvuka ulevi wowote ambao mtu umeshazoea kuwa nao.

Angalia kitu chochote ambacho umezoea kufanya na maisha yako yanategemea kwenye kufanya kitu hicho na chagua kukifanya kwa ukomo kwa kipindi fulani.

Kufunga kula ni moja ya maeneo rahisi ya kuanzia. Unapofunga, kwa kuchagua kuacha kula, hata kama chakula unacho, ni njia nzuri sana ya kuimarisha utashi wako. Na utashi ukiwa imara, tamaa haziwezi kukusumbua, ulevi hauwezi kukushinda na utakuwa na subira ya hali ya juu.

Anza kwa kufunga chakula, au kuchagua kula mara moja kwa siku, na pale unapokuwa na njaa na kutamani kula, jikumbushe kwamba umechagua kutokula, na wewe ndiye utakayeuendesha mwili wako.

Mara zote unaposukumwa kuingia kwenye tamaa, jikumbushe kwamba wewe ndiye unayeuendesha mwili wako na siyo mwili kukuendesha wewe. Ukiweza kuanza na kufunga, mengine yatakuwa rahisi zaidi kwako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Own The Day, Own Your Life (Imiliki Siku Uyamiliki Maisha Yako).

  1. Kuwa na mbadala wa ulevi wako.

Watu huwa wanaendelea na ulevi walionao, wanashindwa kujitoa kwenye ulevi huo kwa sababu hawana mbadala. Kwa mfano kama umezungukwa na marafiki ambao huwa wanafanya kitu fulani, ni rahisi sana kwako kuendelea na ulevi huo kama utaendelea kuwa na marafiki hao.

Kadhalika kama ukivurugwa kidogo unakimbilia kwenye ulevi wako, utaendelea kufanya hivyo kila unapovurugwa.

Unachohitaji ili kuondoka kwenye hali kama hiyo ni kuwa na mbadala wa ulevi wako. Kama ni marafiki, unahitaji kuwa na wengine ambao hawapo kwenye ulevi unaotaka kuukwepa. Kama ni mitandao ya kijamii unahitaji kuwa na kingine cha kufanya ili isiwe kitu cha kwanza kwako kukimbilia. Kuwa na mbadala ambao unakuwezesha kufanya yale muhimu zaidi pale unaposukumwa kwenda kwenye ulevi wako.

  1. Jipe mazoezi ya kujijengea subira.

Tunaishi kwenye dunia ya nipe nikupe, tunaamini tukimpa yeyote kitu basi ana wajibu wa kutupa kitu fulani. Hivyo tumekuwa tunatoa kwa kutegemea kupata. Mtazamo huu umetengeneza hali ya kukosa subira.

Unaweza kujijengea subira kwa kuanza kutoa bila ya kutegemea kupata chochote. Na ili kuhakikisha mtu haoni kama ana deni kwako, toa bila ya kusema umetoa. Unaweza kuchagua kumsaidia mtu kitu ambacho hawezi kukulipa. Mfanyie mtu kitu ambacho hana namna anaweza kukulipa, na ukishafanya sahau.

Usifanye halafu ukaendelea kukumbusha kwamba umefanya, wewe fanya halafu songa mbele na sahau kabisa kama kuna kitu umemfanyia mtu huyo. Fanya zoezi hili mara nyingi uwezavyo na utaanza kuona hali ya subira inajengeka ndani yako.

Rafiki yangu, tamaa, ulevi na kukosa subira ni vitu vitatu vinavyowaangusha wengi na kuwazuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Wewe umeshapata njia ya kuvuka vitu hivi na kuhakikisha haviwi kikwazo kwako. Weka kwenye matendo haya uliyojifunza hapa ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji