Ustoa ni falsafa ya matendo, falsafa ya kuishi maisha bora kwenye nyakati ambazo ni ngumu. Ni falsafa ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 2000 na imeweza kuwasaidia wengi, hasa viongozi wa nchi na hata wanajeshi kupambana na nyakati ngumu kwao.

Uzuri wa falsafa ya ustoa ni kwamba, huhitaji kubadili chochote ulichonacho sasa ili uweze kuishi falsafa hii. Unahitaji tu kubadili fikra zako na kuanza kuchukua hatua tofauti kwenye maisha yako ili kupata matokeo bora kabisa.

Njia bora na rahisi ya kuwa mstoa ni kwa kuchukua hatua,

Kwa mfano;

Pale kila mtu anapopaniki, wewe tulia na fikiri kabla ya kuchukua hatua.

Pale wengine wanaposhawishiwa na tamaa na kuanza kufanya vitu kwa tamaa, wewe endelea kufanya kile unachojua ni sahihi.

Pale wengine wanapotawaliwa na hofu ya kifo, msongo wa mawazo na hatari nyingine, kuwa imara na jiamini.

Kwenye kila ambacho wengine wanasumbuliwa nacho, wewe simama imara, jua kabisa kwamba chochote unachokutana nacho siyo mwisho. Na pia wewe ni imara kuliko chochote unachokutana nacho.

Ustoa ni kuchagua kuishi maisha unayotaka wewe, bila ya kujali nini kinaendelea nje yako. Ni kuchagua kutokutetereka na yale yanayoendelea nje yako, na kutegemea uimara wako wa ndani kukuvusha kwenye changamoto zozote unazokutana nazo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha