Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu ambavyo tunatumia muda wetu kufikiria na kufanyia kazi ni fedha na kipato. Kila mmoja wetu anakazana kufanya kile anachofanya ili aweze kupata fedha ya kuendesha maisha yake.

Lakini pamoja na juhudi kubwa ambazo kila mmoja wetu anaweka, bado wengi wamenasa kwenye lindi la umasikini. Watu wanajitahidi sana, na kwa maneno yao wenyewe watakuambia wamefanya kila kitu ila hakuna hatua wanapiga.

Mpaka wengine wanaishia kuamini labda wao hawakuzaliwa kuwa matajiri, wanaamini kwamba siyo wote tunaweza kuwa matajiri na wao wamewekwa kwenye kundi ambalo hawatafikia utajiri.

Japokuwa nakubaliana na hali kwamba siyo wote wanaweza kuwa matajiri, kwa sababu utajiri unahitaji jitihada za ziada, sikubaliani na unachojiambia kwamba wewe ni mmoja wa wale ambao wapo wameletwa duniani wasiwe matajiri.

Nimekuwa naamini kitu kimoja, pale tunapofika au kutokufika kunachangiwa na vitu viwili; UNACHOJUA na HATUA UNAZOCHUKUA.

Kama wewe ni masikini basi kuna vitu hujui kuhusu fedha na kuna hatua ambazo hujachukua kuhusu fedha.

Nina maana kwamba, ukiwa na MAARIFA SAHIHI halafu ukachukua HATUA KUBWA lazima utapata matokeo makubwa kwenye maisha yako.

Leo napenda tukumbushane mambo matatu muhimu kuhusu fedha ambayo wengi hawajui au hawaweki msisitizo na hilo linawapelekea kunasa kwenye lindi la umasikini.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Inawezekana ulishasikia tena mambo haya matatu, lakini hujafanyia kazi na ndiyo maana hupigi hatua.

Leo nakukumbusha tena, na kukupa hatua za kuchukua ili uweze kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.

Moja; hujui kuhusu kupata fedha.

Kitu cha kwanza usichojua kuhusu fedha ni jinsi ya kuipata. Na hapa unaweza kuona nakutania, kwamba iweje hujui kuhusu kuipata fedha wakati maisha yako yote umekuwa unafanya kazi kwa juhudi ili upate fedha? Na hapo ndipo tatizo linapoanzia.

Kile unachojua kuhusu kupata fedha siyo sahihi au unajua siyo kwa ukamilifu. Kwa mfano ulifundishwa kwamba ukisoma vizuri, ukafaulu, utapata kazi nzuri itakayokulipa vizuri. Umefanya yote hayo na kazi umeipata, lakini haikulipi kiasi cha wewe kuweza kutimiza mahitaji yako. Sasa wewe unachagua kufanya nini? Unakimbilia kukopa, ukijiambia kwamba njia pekee ya kupata unachotaka ni kukopa.

Kuna vitu viwili ambavyo hujui kuhusu kupata fedha.

Cha kwanza hujui kwamba fedha ni matokeo ya thamani unayozalisha. Kwamba kipato unachopata sasa ni matokeo ya thamani unayotoa. Kama kipato ni kidogo basi thamani unayotoa kwa wengine ni ndogo. Hivyo njia pekee ya kuongeza kipato chako ni kuongeza thamani unayoitoa kwa wengine.

Cha pili hujui kwamba mfereji mmoja wa kipato hauwezi kumaliza shida zako. Hakuna mtu amewahi kumaliza shida zake zote kwa mshahara tu, au biashara moja pekee. Unahitaji kuwa na mifereji mingi zaidi ya kipato. Unahitaji kuwa na njia mbalimbali za kuingiza kipato kiasi kwamba kama njia moja itasumbua, basi njia nyingine zitaendelea kukuingizia kipato.

Ongeza thamani yako kwa wengine na ongeza njia zako za kuingiza kipato na hilo litakuwezesha kuondoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri.

SOMA; Aina Tatu Za Ukomo Uliojiwekea Kwenye Kipato Na Njia Tano Za Kuondoa Ukomo Kwenye Kipato Chako Ili Kufikia Uhuru Wa Kifedha.

Mbili; hujui kuhusu kuweka fedha.

Nyoosha mkono hapo ulipo kama kila ukiwa huna fedha unakuwa na mawazo mazuri sana, lakini ukizipata unasahau mawazo yote mazuri, unatumia zinaisha na ndiyo unakuja kukumbuka mawazo yake. Endelea kunyoosha mkono wako kama kila ukiwa na fedha ndiyo matatizo mapya yanaibuka, watu wanaumwa, ndugu wanahitaji na hata vitu vinaharibika.

Kwa wengi, fedha ikipatikana huwa haikosi kitu cha kufanya, hivyo ukiwaambia wanapaswa kuweka akiba, watakushangaa. Niwekeje akiba wakati fedha yenyewe hata haitoshi? Nitawekaje akiba wakati bado nahitaji kwenda kukopa ili kutimiza mahitaji yangu?

Jambo la pili muhimu unapaswa kujua kuhusu fedha ni kuiweka fedha yako, yaani kuwa na akiba kwenye kila kipato unachotengeneza. Usikubali fedha yoyote ipite kwenye mikono yako na uishie kuwapelekea wengine. Unahitaji kubaki na sehemu ya fedha hiyo kama alama kwako kwamba unaweza kudhibiti kipato chako na hata kukikuza zaidi.

Na kwa sababu umeshajifunza kwamba fedha kwako huwa haikai, usijiambie unatumia ikibaki uweke akiba. Badala yake, unapopokea fedha yako, weka kwanza akiba kabla hata hujaanza kutumia. Tenga fungu la akiba halafu inayobaki ndiyo utumie.

Siri kuu ya kuweka akiba ni hii, weka akiba kabla ya matumizi, usitumie halafu ukasema ikibaki utaweka akiba, haitabaki. Akiba yako weka eneo ambalo haitakuwa rahisi kwako kuitumia pale unapokuwa na shida. Nimekuwa nasema unahitaji kuwa na gereza la kufungia fedha yako, kiasi kwamba japo ni yako, lakini huwezi kuipata.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kudhibiti Mzunguko Wako Wa Fedha, Kuituliza Fedha Mfukoni Na Kuongeza Faida Kwenye Biashara.

Tatu; hujui jinsi ya kutumia fedha kuzalisha fedha zaidi.

Jambo la tatu usilojua kuhusu fedha ni kuitimua fedha yako kuzalisha fedha zaidi. Watu wengi wamezoea kutumia nguvu zao kuzalisha fedha. Hili linafanya kazi vizuri ukiwa kijana na mtu mzima, ambaye una nguvu za kufanya kazi. Lakini pale unapofika uzee, na nguvu za kufanya kazi zinapungua, ndiyo unagundua kwamba hukujipanga vizuri.

Unahitaji kutengeneza njia ya fedha zako kuzalisha fedha zaidi, hata kama nguvu zako hazipo. Na hapa ndipo uwekezaji unapoingia. Uwekezaji ni njia ya fedha yako kufanya kazi na kuzalisha zaidi huku wewe ukiendelea na mambo yako mengine.

Ile fedha unayoiweka akiba kwenye kipato chako, unapaswa kuiwekeza kwenye maeneo yanayozalisha fedha zaidi. Unahitaji kuchagua uwekezaji unaouelewa na unaoweza kuufuatilia ili kuweza kukuza zaidi fedha zako na kujitengenezea utajiri.

Kumbuka uhuru wa kifedha ni pale unapoweza kuishi utakavyo hata kama hufanyi kazi moja kwa moja. Na huwezi kufikia uhuru wa kifedha kama huna uwekezaji. Unaweza kuwa tajiri ka kufanya kazi, lakini huwezi kuwa na uhuru wa kifedha kwa kufanya kazi, unahitaji kuiwezesha fedha yako ikufanyie kazi.

Rafiki yangu, hayo ndiyo mambo matatu muhimu niliyopenda kukujulisha na kukukumbusha leo kuhusu fedha. Jifunze mambo haya kwa kina na anza kuchukua hatua sasa hivi kwenye maisha yako ili ujiweke vizuri kifedha.

Kila la kheri.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji