Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye kuongeza kipato na hata mafanikio kwa ujumla, tunatumia kanuni ya asili ya kilimo. Kwamba huwezi kuvuna kabla hujapanda. Mkulima yeyote mwenye akili timamu, anajua ya kwamba ili aweze kuvuna mazao mazuri, lazima awekeze kwanza. Lazima aweke nguvu kuandaa shamba, lazima aweke mbegu, lazima ahudumie mimea hiyo na ndiyo mwishoni aweze kuvuna.

Lakini kwenye maisha ya kawaida, kwenye kazi, biashara na hata mahusiano, watu wanaona kama kanuni hiyo haihusiki au haifanyi kazi. Watu hawataki kuwekeza kwanza na kunufaika baadaye. Watu wanataka wapate kwanza ndiyo wawekeze. Hili ni jambo la kushangaza, lakini ndivyo wengi wanavyofanya mambo yao.

Kwa mfano, kama unataka kulipwa zaidi, lazima utumie kanuni ya asili ya kilimo, lazima uwekeze kwanza, lazima upande kwanza kabla ya kuvuna. Lakini wengi wamekuwa hawapo tayari kutumia kanuni hiyo ya kuwekeza kwanza. Wengi wanataka kipato kiongezeke kwanza ndiyo wawekeze.

Wengi wanafanya kazi za kawaida na wanaishia kulipwa kawaida sana. Wanajiambia kama wakianza kulipwa vizuri basi nao watafanya kazi bora zaidi. Ambacho hawajui ni kwamba, wanahitaji kuanza kufanya kazi bora kwanza kabla hawajalipwa vizuri. Ili ulipwe zaidi ya unavyolipwa sasa, lazima kwanza ufanye zaidi ya unavyofanya sasa. Lazima ufanye kazi bora zaidi na ya thamani zaidi kuliko unavyolipwa sasa.

Kadhalika kwa wale waliopo kwenye biashara, wengi wamekuwa wakisema kama wateja wangewalipa zaidi basi nao wangetoa huduma bora zaidi. Wanachosahau ni kwamba wanapaswa kuanza kutoa huduma bora zaidi ndiyo wateja waweze kuwalipa zaidi.

Rafiki, kanuni ya asili ya kupanda kabla ya kuvuna inafanya kazi kwenye kila eneo la maisha yetu. Hata kwenye mahusiano yetu, wengi wanaharibu mahusiano yao kwa sababu wanataka wengine wafanya vitu fulani kwanza ndiyo na wao wafanye. Lakini kama wangechukua hatua na kuanza kufanya wao, basi wengine nao wangefanya bila ya shida yoyote.

Kutaka ulipwe vizuri kwanza ndiyo na wewe ufanye vizuri ni sawa na kwenda shambani na kusema wewe shamba nipe mazao na baadaye nitakupa mbegu. Au kuchukua kuni na kuziweka jikoni na kusema haya kuni nipeni moto. Unajua kabisa ni kitu cha kushangaza, lakini unaendelea kufanya hivyo kila siku. Unajua kabisa hata uwe na kuni nzuri kiasi gani, kama hutaanza kwa kuwekeza moto kidogo, kuni hizo hazitakupa moto kabisa.

Usomaji

Rafiki yangu, nina imani umeelewa umuhimu wa wewe kuwekeza kwanza kabla hujategemea kuvuna. Ni muhimu mno, kabla hujajiuliza napata nini, tafadhali jiulize kwanza unatoa nini. Na kabla hujategemea kupotea, toa kwanza. Tumia kanuni hii kwenye kila eneo la maisha yako, na utashangaa kwa jinsi ambavyo utaweza kupata chochote unachotaka.

Kanuni rahisi ya kukuwezesha wewe kupata chochote unachotaka, ni kutoa kwanza kile ambacho unapaswa kuwekeza kabla ya kupata. Unataka mazao lazima uwekeze kwanza nguvu na mbegu, unataka upendo lazima kwanza uwekeze upendo kwa wengine, unataka wateja zaidi lazima kwanza uwahudumie wateja ulionao vizuri.

SOMA; Vitu Hivi Vitatu Usivyovijua Kuhusu Fedha Ndiyo Vinakuzuia Wewe Kufika Kwenye Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Pamoja na urahisi na uhakika wa kanuni hii kukupatia chochote unachotaka, najua wasiwasi wa wengi uko hapa; naweza kufanya sana lakini nisilipwe. Wengi wana wasiwasi kwamba wanaweza wakafanya sana kazi lakini waajiri wao wasiwajali, au wanaweza kutoa huduma bora sana kwa wateja na wasijali kuwalipa kama wanavyotaka.

Ninachoweza kukuambia rafiki yangu ni hiki, wewe fanya, wewe wekeza nguvu, wewe toa thamani, na kazana kufanya hivyo kila siku. Hata kama wale unaowahudumia sasa, wale unaowafanyia kazi sasa hawataona, jua kuna wengine wataona, na hao wengine watakuwa tayari kulipa kwa kadiri unavyostahili kulipwa, kulingana na jinsi unavyofanya.

Wewe kazi yako ni kufanya, na kama wale ulionao sasa hawatakulipa, basi jua dunia itakulipa. Dunia haitupi yule ambaye anatengeneza thamani kubwa. Kama ambavyo wanasema jembe halimtupi mkulima. Mkulima anaweza asivune vizuri kwenye msimu fulani, lakini hilo halimfanyi aache ukulima. Badala yake msimu mwingine anapanda vizuri na kuweka juhudi zaidi na anavuna kwelikweli.

Tumia kanuni ya kutoa kwanza kabla hujapokea, na elewa kama ulionao hawatathamini unachotoa, wapo wanaoona na watakuwa tayari kukulipa kadiri unavyostahili.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL