“Everyone thinks of changing the world, but no one thinks of changing himself.” — Leo Tolstoy

Siku mpya,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUIBADILI DUNIA NA KUJIBADILI MWENYEWE…
Watu wamekuwa wanajipa majukumu magumu sana kwao, ambayo yapo kabisa nje ya uwezo wao, na wakati huo wana majukumu yao ambayo yapo ndani ya uwezo wao ila wanayakimbia.

Moja ya majukumu magumu watu wanajipa ni kuibadili dunia.
Hakuna anayeweza jukumu hili,
Hakuna anayepanga kuibadili dunia akashinda.
Dunia haitaki kubadilishwa.

Jukumi jingine ambalo wengi wanajipa na linawashinda ni kukazana kuwabadili wengine.
Ni kitu kingine ambacho hakiwezi kutokea kabisa.
Kwa sababu watu wanaweza kukubaliana na wewe kinafiki, lakini hawabadiliki kwa sababu ya wewe.

Jukumu rahisi ambalo kila mtu analikimbia ni kubadilika yeye mwenyewe.
Hili ni jukumi rahisi sana, ambalo lipo ndani ya uwezo wakila mtu.
Ila wengi hawapendi kubadilika, wengi wanapenda mazoea na ndiyo maana wanakwepa kubadilika.

Rafiki yangu, kila unapokaa na kujiambia nataka kuibadili dunia, nataka kumbadili mtu fulani, achana kabisa na mawazo hayo, kisha jiulize ni maeneo gani nahitaji kubadilika kwenye maisha yangu.

Uzuri ni kwamba, ukianza kubadilika wewe, basi na wale wanaokuzunguka wanaweza kuchagua kubadilika, na wale wanaowazunguka pia wakabadilika, na ghafla dunia nzima ikachagua kubadilika.
Hapo hujainadili dunia, umejibadili mwenyewe na dunia ikajibadili, kupitia wewe.

Kuwa tayari kubadilika, kila siku hakikisha unakuwa bora zaidi ya jana. Na kama mabadiliko yako yatakuwa mema, dunia itakuunga mkono.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya mabadiliko kwako binafsi.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha