Rafiki yangu mpendwa,

Nimekuwa nakuambia hakuna siri yoyote ya mafanikio. Yeyote anayekuambia ana siri ya mafanikio, anakuambia vitu ambavyo vipo wazi, lakini wengi hawavizingatii.

Hivyo kwenye makala hii, nikuhakikishie kwamba sitakuambia kitu ambacho hukijui kabisa, lakini nitakisisitiza kwako kwa namna ambayo hujawahi kusikia kwenye maisha yako.

Ipo siri moja kubwa ya mafanikio ambayo hakuna mtu ambaye yupo tayari kukuambia wazi wazi.

Na hata wale ambao wamefanikiwa sana kwa kutumia njia hii, huwa hawaisemi, kwa sababu watawaumiza wale watakaosikia.

Iko hivi rafiki yangu, watu wanapenda sana ulaini, watu wanapenda sana kuhukumu na pale mtu anapoonekana kuishi tofauti na watu walivyozoea kuishi, anaonekana mtu wa ajabu.

Hivyo wale waliofanikiwa wanajua hili, na kwa sababu hawataki kusumbuana na watu, wanachagua kukaa kimya, kuendelea kutumia kile kinachowasaidia huku wengi wakiendelea kukimbizana na vitu ambavyo vinawapotezea muda na haviwaletei mafanikio.

weka kazi

Siri kubwa ambayo siyo siri, lakini nimejipanga kuisisitiza sana kwako leo ni hii; UNAHITAJI KUFANYA KAZI SANA KULIKO WENGINE WOTE WANAOFANYA UNACHOFANYA. Wazungu wanasema OUTWORK everyone. Unajisikiaje unaposikia maneno kama hayo? Kama haijaingia vizuri niongeze msisitizo.

Kwa kawaida, watu wanafanya kazi kwa wastani wa masaa 40 kwa wiki, yaani masaa nane kwa siku, siku tano za wiki. Hata wale wanaofanya siku sita au saba, jumla hawazidi masaa 60. Sasa kama unataka mafanikio yasiyo ya kawaida, huwezi kuyapata kwa masaa hayo ya kazi kwa wiki.

Ninachomaanisha ni kwamba, hutaweza kupata mafanikio makubwa kwa kufanya kazi kama wengine wanavyofanya, kwa muda ambao wengine wanafanya. Ili upate mafanikio makubwa, unahitaji kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya wengine, mara mbili ya masaa wanayofanya wengine.

SOMA; Kitu Ambacho Kitakuonyesha Kama Unafanikiwa Au Hufanikiwi Kwa Kitu Unachokifanya.

Na kwa kuanzia, hayo ni masaa yasiyopungua 100 kwa siki, au masaa 14 mpaka 15 kila siku kwa siku saba za wiki.

Hii ina maana kwamba, kazi itakuwa kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako, na vitu vingine vitahitaji kusubiri sana kwa sababu una kazi za kufanya.

Na pia ina maana kwamba, maisha ya kijamii unaweza usiwe nayo kabisa. Kwamba eti una muda wa kuangalia michezo, kusoma na kuangalia habari, kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, kwenda kwenye sehemu za starehe na kuhudhuria kila aina ya kikao ambacho hakuna umuhimu mkubwa. Hivyo vitu utavisahau kabisa kwenye maisha yako.

Bado hujashawishika kwa nini wengi hawakuambii hili? Najua hapa unaposoma sasa unajiambia hapana, hayo siyo maisha, ni bora nisifanikiwe na niwe na maisha mazuri ya kijamii kuliko kufanikiwa kwa kufanya kazi muda mrefu hivyo.

Na hakuna tatizo kabisa kwenye hilo, muhimu tu ni uache kujidanganya na uishi maisha kama ulivyochagua.

Natoa ujumbe huu wa kwale wanaojidanganya na kudanganya wengine kwamba wanataka kufanikiwa sana, halafu eti ni mashabiki wa mpira, wasipoangalia mpira wanajisikia vibaya, eti mtu anakunywa kabisa pombe na kulewa na kujiambia atafanikiwa. Hicho kitu hakipo rafiki yangu.

Mafanikio makubwa hayaji kwa maneno au kutaka, yanakuja kwa kazi, tena siyo kazi ya kitoto. Kazi hasa, na kuna maisha mengine itabidi uyasahau kabisa kutokana na kazi utakazokuwa unafanya.

Na ili kuweka mambo sawa, nikumbushie tu;

  1. Ninaposema kazi simaanishi kazi ya kuajiriwa, bali chochote unachofanya. Iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara, unahitaji kuweka kazi na muda.
  2. Ninaposema mafanikio makubwa simaanishi fedha pekee na utajiri, namaanisha kufikia kile ambacho kipo ndani yako. Kwamba kila mtu ana uwezo mkubwa sana uliopo ndani yake, lakini ili kuufikia, kazi kubwa sana inahitajika.
  3. Mafanikio makubwa siyo kwa kila mtu, kwa sababu siyo kila mtu yupo tayari kuumia ili afikie mafanikio makubwa. Hivyo kama wewe siyo mmoja wa hao, jitambue kabisa na acha kujidanganya. Pia acha kulalamika kwamba maisha yako huyapendi, jua umechagua maisha ya kawaida, ishi hayo na usisumbue wengine.

Ni hayo machache kwako leo rafiki yangu, kama yamekufanya ujisikie vibaya, basi ujue kuna mahali unakosea. Kama umekua unajiambia utafanikiwa halafu unafanya vitu visivyoendana na mafanikio, acha kujidanganya, labda ukubali kuyaishi mafanikio au ukubali kuishi ukawaida.

Maisha ni yako, chaguo ni lako, muhimu ni uache kujidanganya.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji