Rafiki yangu mpendwa,

Uzuri wa zama tunazoishi sasa ni kwamba hamasa ni rahisi sana kupatikana, hasa hamasa kutoka kwa wengine. Hii ni kwa sababu kuna maarifa na taarifa za kutosha kuhusu wale waliofanikiwa.

Lakini mara nyingi taarifa zinazowahusu wale waliofanikiwa sana, huwa zinaonesha walipoanzia ambapo ni chini sana, na walipofika ambapo ni juu kabisa.

Wale wanaoanzia chini, wanapata hamasa kubwa sana kwamba kama kuna mwingine alianzia chini kama wao na akafanikiwa, basi na wao pia wanaweza kufanikiwa sana.

Wanaanza kuwa na ndoto kubwa, wanakuwa na mipango mikubwa na kupanga kuchukua hatua kubwa. Na yote haya ni mazuri sana katika kuhakikisha mtu unafanikiwa.

Lakini tatizo linakuja pale wengi wanapoanza kuchukua hatua, wanakutana na ugumu ambao unawakatisha wengi tamaa. Na wale wasiokata tamaa kwa ugumu, wanakutana na kitu ambacho hawakukitegemea.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Kitu hicho ni ukuaji mdogo sana wanaopata licha ya kuweka juhudi kubwa. Wanakuwa wakifikiri kwa kuwa wanajua njia ya mafanikio, basi wanaweza kuharakisha sana, hawahitaji kusubiri zaidi. Na hapo ndipo wanapokata tamaa, kwa sababu wanaweka juhudi kubwa sana, lakini matokeo wanayopata ni madogo sana.

Wengi wanashawishika labda ipo siri ambayo waliofanikiwa wanaificha, hawaitoi kwao, na ndiyo maana hawapati matokeo makubwa haraka. Hivyo wanaacha kile wanachofanya na kuanza kukimbizana na fursa wanazoambiwa zinaleta mafanikio haraka. Na hapo ndipo wanapopotea zaidi.

Rafiki yangu, kwa kuwa nakupenda sana wewe na ninachopenda zaidi ni wewe ufanikiwe, kwa sababu najua kadiri unavyofanikiwa wewe ndivyo na mimi nafanikiwa zaidi, ninakushirikisha siri ambayo siyo siri, lakini ni muhimu sana kwa mafanikio yako kama unaanzia chini kabisa.

SOMA; Hii Ndiyo Siri Kubwa Ya Mafanikio Ambayo Hakuna Mtu Aliye Tayari Kukuambia Wazi Wazi.

Siri hiyo isiyokuwa siri, nasema hivyo kwa sababu ni kitu kilicho wazi, lakini wengi hawakichukulii hatua, ni kwamba unahitaji kupiga hatua moja kwa wakati.

Naomba nieleze taratibu ili asibaki nyuma mtu yeyote, njia pekee ya kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako, kama unaanzia chini kabisa, ni kupiga hatua moja kwa wakati, na kuweka kazi kubwa sana kwenye kila hatua unayochukua.

Ndiyo unaweza kupata mafanikio makubwa kama unavyotaka wewe, lakini hayatatokea kama ajali, hutalala masikini na kuamka tajiri. Badala yake utahitaji kuweka kazi kubwa, kisha kuwa mvumilivu wa kupiga hatua moja kwa wakati na hivyo ndivyo utakavyoweza kufanikiwa.

Kazi inahitajika sana, tena kazi ya maana na siyo ya kitoto, kazi ambayo haijazoeleka na wengine.

Subira ni muhimu sana, kama unafikiria ndani ya mwaka mmoja au miwili utakuwa umepata mafanikio makubwa unayotaka unajidanganya. Kwa kiwango cha chini kabisa fikiria miaka kumi, na kuwa tayari kuweka juhudi kubwa kwa angalau miaka kumi kabla hujaanza kuona matokeo makubwa kama unavyotaka wewe.

Unachohitaji ni kuwa kwenye njia sahihi, kuwa na maarifa sahihi, kuchukua hatua kubwa na utakachokuwa unasubiri ni matokeo makubwa pekee.

Tuseme umechagua kuwa mwandishi, hakuna anayekujua, na unataka kuwa mwandishi mkubwa kwa sababu una ujumbe utakaowasaidia sana wengi. Unahitaji kuanza na msomaji mmoja kwa wakati. Kaa chini na mwandikie mtu mmoja ambaye unajua ana uhitaji wa ujumbe ulionao. Mtumie mtu huyo ujumbe huo uliomwandikia, tushukuru sasa tuna teknolojia rahisi ya kufanya hivyo, unaweza kutumia ujumbe wa simu, ujumbe wa wasap, ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, na hata blog. Mtumie msomaji mmoja na kisha msaidie kutatua changamoto alizonazo, kisha yeye atawaambia wengine na ndivyo utakavyoenda mpaka kufikia lengo lako.

Kadhalika kama unataka kuwa mfanyabiashara mkubwa sana, huna pengine pa kuanzia zaidi ya kuanza na mteja mmoja mwenye uhitaji na ambaye unaweza kumhudumia vizuri kwa kile unachotoa. Mpe mteja huyo mmoja huduma bora kabisa na kisha yeye atakuletea wateja wengine wengi. Na pia utatumia kuridhika kwa mteja huyo mmoja kuwafikia wateja wengi zaidi.

Hakuna kitu chochote hapa duniani ambacho huwezi kuanza na mtu mmoja, huwezi kuanza na hatua moja na ukafanikiwa sana. Tunadanganywa sana na dunia kwamba mafanikio yanapaswa kuwa ya haraka na yasiyotumia nguvu, mwishowe tunaishia kuwa wateja wa kuwanufaisha wengine huku sisi tukihangaika sana.

Ukifanyia kazi hichi nilichokushirikisha hapa leo, utaokoa wastani wa miaka kumi ambayo wengi wanapoteza kwenye maisha yao, wakihangaika na njia za mkato. Wewe tumia ndefu, tumia njia ya kuanza na mteja mmoja kwa wakati. Tumia njia ya kuweka kazi na kuwa na uvumilivu na ipo siku watu watasema una bahati sana kwa kuwa umeanzia chini na sasa upo juu. Ni kweli utakuwa na bahati, maana wengi hawajui kile ulichokipitia mpaka kufika pale.

Ni hatua moja kwa wakati rafiki yangu, msomaji mmoja kwa wakati, mteja mmoja kwa wakati, shabiki mmoja kwa wakati. Safari ya mafanikio ni hatua moja baada ya nyingine, kuwa tayari kupiga hatua hizi na achana na njia za mkato zitakazopoteza muda wako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL