Tabia ya binadamu ni moja, tunapenda kuamini vitu na kisha kuvizoea.
Kadiri vitu vinakwenda kama tulivyozoea viende, maisha yetu ni mazuri.
Lakini vitu vinapokwenda tofauti na tulivyozoea, wakati tumeshaweka matumaini yetu kwenye vitu hivyo, hapo ndipo mgogoro unapoanzia.
Hivi ndivyo unavyopaswa kwenda na wateja wako kwenye biashara yako.
Wafanye wateja wako wakutegemee wewe moja kwa moja, na wasiwe na wasiwasi wowote juu ya kile unachowapatia.
Na fanya kadiri inavyopaswa kufanywa (na siyo kadiri ya uwezo wako) kuhakikisha mteja anapata kile anachotegemea kupata kwako.
Usijiambie kwa furaha kabisa kwamba umefanya kadiri ya uwezo wako, au kitu kipo nje ya uwezo wako. Kama mteja umeshamtengenezea mategemeo fulani kwenye biashara yako, kufa ukitekeleza mategemeo hayo.
Nasema hivi kwa sababu naona wafanya biashara wengi wanakuwa wavivu sana. Wanaendesha biashara kwa mazoea na kuona wateja watakuja tu. Wateja wanakuja na mategemeo fulani wanaondoka wakiwa wamevunjwa moyo. Na kinachotokea ni kwamba wakati mwingine wanakosa imani ya kuja tena kwenye biashara ile.
Usiwe mvivu, fanya kila kinachopaswa kufanya kuhakikisha mteja anaendelea kujenga imani kubwa na biashara yako. Maana hilo pekee ndiyo muhimu kwa biashara yako, ukilitekeleza, hutakosa wateja kamwe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,