Mwanafalsafa Socrates alinukuliwa kusema maisha ambayo hayapimwi wala kuhojiwa hayana maana ya kuishi.
Haijalishi tuna misingi mizuri kiasi gani tunayoishi kwenye maisha yetu, mara kwa mara tutajikuta tunaanguka. Tunajikuta tunafanya vitu vinavyoenda kinyume na misingi yetu.
Siyo rahisi kuona vitu hivyo kama mtu utakuwa unafanya kwa mazoea. Kama mtu utakuwa hujichunguzi, hujihoji na kujipima kila mara, ni rahisi sana kuondoka kwenye njia yako ya mafanikio.
Kwa mfano, moja ya vitu vinavyowazuia wengi kupiga hatua ni kujikuta wana vitu vingi vya kufanya kuliko muda na nguvu walizonazo za kufanya.
Watu wanapoteza muda na maisha yao, kufanya vitu ambavyo hawapendi kuvifanya ili kuwaridhisha watu ambao hawawaheshimu na kupata vitu ambavyo hata hawavitaki.
Ukishajiambia kwenye maisha yako kwamba bila ya watu fulani au vitu fulani hayawezi kwenda, unajiweka kwenye vifungo, ambavyo vitakupelekea ufanye vitu usivyotaka, ili upate usichotaka.
Ni muhimu sana kujipima kwenye kila unachofanya, na kuona kama kweli kinachangia kwenye kile unachotaka kwenye maisha yako.
Kabla hujasema ndiyo kwa yeyote, tafadhali sana jiulize je hicho unachotaka kusema ndiyo ndiyo kitu muhimu zaidi kwenye maisha yako. Kama jibu ni hapana basi usipoteze muda wako, sema tu HAPANA hata kama itamuumiza mtu.
Wengi wamekuwa wanaogopa kuwaumiza wengine na hivyo wanaishia kuumia wao wenyewe.
Chukua dakika chache kujipima na kujichunguza leo, je kuna chochote unachofanya kwa sababu unataka tu kuwaridhisha wengine na siyo kitu unachotaka kufanya? Kama jibu ni ndiyo, jiondoe mara moja kwenye mtego huo kabla haujaendelea kutafuna maisha yako.
Maisha uliyonayo hapa duniani ni haya tu, na yana ukomo, usiyapoteze kwa mambo yasiyo muhimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,