Kuna wakati watu wanafanya vitu ambavyo unashindwa kabisa kuvielewa.

Unashindwa kuelewa kwa nini wamefanya kama ambavyo wamefanya, maana hukutegemea wafanye hivyo.

Sasa njia mbaya kabisa ya kujua kwa nini ni kuwauliza kwa nini wamefanya walichofanya.

Kwa sababu hakuna hata mmoja atakayekupa jibu sahihi kwa nini amefanya kile alichofanya, ambacho siyo kitu sahihi kufanya.

Wewe muulize mtu yeyote uliyemkamata akiiba kwa nini ameiba, au aliyesaliti kwa nini amesaliti. Sababu yoyote atakayokupa haitakuwa sababu sahihi.

Kuuliza mtu kwa nini amefanya kitu ambacho siyo sahihi hakutakupa jibu sahihi la kwa nini amefanya hivyo.

Njia pekee ya kupata jibu sahihi kwa nini mtu amefanya kitu fulani, ni kuangalia motisha na hamasa iliyompelekea kufanya kitu hicho.

Angalia kwa yeye kufanya kile alichofanya, ananufaika vipi? Au anakimbia maumivu gani?

Kwa sababu chochote tunachofanya kwenye maisha yetu, ni kwa sababu mbili, labda tunataka kupata tunachotaka au tunakwepa maumivu au kupoteza.

Ukiangalia vizuri kwenye chochote kile mtu anafanya, utaona msukumo hasa umeanzia wapi na hapo unaweza kuchukua hatua sahihi.

Lakini ukiuliza tu, utabaki na maswali yako na hutopata jibu sahihi.

Angalia msukumo, angalia matokeo ambayo watu wanatarajia kupata kwa kile wanachofanya na hapo utapata jibu sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha