Rafiki yangu mpendwa,
Wanasema mambo yote yakiwa sawa, watu wanapenda kufanya biashara na marafiki zao. Na hata mambo yote yasipokuwa sawa, bado watu wanapenda kufanya biashara na marafiki zao.
Huduma ambazo mteja wako anapata kwenye biashara yako, zinaweza kuchangia biashara kukua zaidi au kufa. Kama mteja anapata huduma nzuri, ataiamini biashara na kuitegemea. Kama anapata huduma mbovu atashindwa kuiamini biashara na hatorudi tena.
Pia lazima ujue kwamba mteja anaponunua kile unachouza anachukua hatua ya hatari sana kwenye maisha yake. Kwa sababu fedha anayokupa wewe, hawezi tena kuitumia kwa shughuli zake nyingine.
Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha kwamba mteja anapata kile anachotarajia kupata, na huduma bora sana.
Katika kuimarisha huduma ambazo mteja anapata kwenye biashara yako, zingatia mambo haya matano.
Moja; uelewa wa mteja.
Mteja anapaswa kuelewa ni kwa namna gani kile unachokwenda kumuuzia kitatatua matatizo yake au kutimiza mahitaji yake. Kama mteja hawezi kuelewa hilo, hataweza kununua.
Hivyo unapomwelezea mteja kuhusu biashara yako, usikazane kueleza sifa za unachouza ukilinganisha na vingine. Bali kazana kumwambia inatatuaje matatizo yake, na inafanyaje maisha yake kuwa bora.
Mteja mwenye uelewa mzuri wa namna unachouza kinaweza kumsaidia, atakuwa tayari kununua.
Mbili; kuweza kutofautisha.
Kuna watu wengi wanamwahidi mteja huyo kwamba akifanya nao biashara basi maisha yake yatakuwa bora sana. Je ni kitu gani kitamfanya mteja awaache hao wengine wote na kufanya biashara na wewe?
Lazima mteja awe na njia ya kuweza kukutofautisha wewe na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara unayofanya.
Mteja anahitaji kuwa na njia ya kujua kwamba wewe ndiye mtu sahihi kwake ukilinganisha na wafanyabiashara wengine.
Angalia kipi cha thamani kwa mteja ambacho hawezi kukipata kwingine, kisha mweleze wazi. Hii itakusaidia kumshawishi mteja anunue.
Tatu; kinachotokea anapokuwa tayari kununua.
Mteja anapokuwa tayari kununua, ni nini kinatokea kwake na kwako? Unaweza kuona hili ni swali rahisi, lakini wengi sana wanafanya makosa ambayo yanapoteza imani ya mteja na anaahirisha zoezi la kununua.
Unahitaji kujua ni wakati gani mteja yupo tayari kununua na kukamilisha manunuzi yake. Kila wakati unaweza kuona kama mteja ana wasiwasi fulani, lakini ukishazijua tabia za wateja wako vizuri, utajia wakati gani ameshafikia maamuzi ya kununua na hapo ukampa uhakika zaidi kwamba hatua anayokwenda kuchukua ni sahihi kabisa kwenye maisha yake.
SOMA; Njia Tatu Za Kumuuzia Mteja Ambaye Amekataa Kununua. Jifunze Hapa Ili Usishindwe Kuuza Tena.
Nne; kitakachotokea baada ya kununua.
Hakuna kitu kinachomuumiza mteja wako kama akifikiria nini kitakachotokea baada ya kuwa amenunua. Anafikiria vipi kama alichonunua hakitafanya kazi kama alivyotegemea. Pia vipi kama kitaharibika kabla hata hajatumia vizuri. Hili linaweza kumfanya mteja asite kununua.
Kumpa uhakika mteja kwenye hili unahitaji kutoa uhakika, kwamba mambo hayaishi pale anaponunua, bali ndiyo kwanza yanaanza. Unahitaji kumweleza mteja wako kwamba akishanunua, mahusiano yenu ndiyo yanaimarika zaidi.
Unahitaji kumpa uhakika mteja wako kwamba kama alichonunua hakitamfaa basi anaweza kurudi na akapata kingine. Na kama kitaharibika ndani ya muda fulani, basi anaweza kurudi na akapata kingine. Hali hii ya uhakika inaondoa wasiwasi kwa mteja na kumfanya awe tayari kutoa fedha na kununua.
Tano; je anaweza kuwaambia wengine nao wakaja?
Watu hawapendi kuwaangusha watu wao wa karibu, hivyo kama mteja hatapata huduma nzuri kama alivyotegemea, hatawaambia wengine waje kwako. Na tena atachukua hatua ya kuwapa tahadhari kwamba wawe makini na wewe.
Hivyo moja ya majukumu yako makubwa ni kuhakikisha mteja anasukumwa kuwaambia wengine ili nao waje wapate huduma bora kama aliyopata yeye. Ukimpa huduma bora kabisa, halafu ukamwomba awaambie wengine, atafanya hivyo na biashara yako itakua zaidi.
Zingatia mambo hayo matano kwenye huduma unazotoa kwa wateja wako, na utaimarisha sana mahusiano yako na wateja wako na kuikuza zaidi biashara yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha