Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto ambapo tunapeana hatua za kuchukua ili kuweza kuvuka changamoto zozote ambazo zinatuzuia kupiga hatua kwenye maisha yetu.

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujifunza hatua za kuchukua pale wateja wanapokuacha na kwenda kwa wafanyabiashara wengine.

Wote tunajua kwamba bila ya wateja, hakuna biashara. Hivyo jukumu muhimu la kila mfanyabiashara ni kutengeneza wateja ambao watakuwa wanaitegemea biashara hiyo.

Sasa zipo nyakati ambazo wateja wako wanaweza kukuhama na kwenda kwa wafanyabiashara wengine. Unapokuwa kwenye wakati kama huu, jua kabisa kuna makosa unafanya na unahitaji kuchukua hatua haraka ili kuinusuru biashara yako.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Kabla hatujaona hatua hizo za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuomba ushauri kwenye hili;

“Ni mpigaji picha za mnato, uwezo ni mzuri wa upigaji na kamera ni Fuji x16. Wakati wa sherehe kama mahafali wateja wanaweza Kuniacha na kwenda kwa wenye kamera ndogo. Je, tatizo langu ni lipi? Pia naendelea kazi hii sana kwani nimezoea kwa Miaka 10 sasa. Natamani kufungua studio ya kuanzia, je mambo gani nizingatie?” – Filbert M.

Kama wateja wanakuacha na kwenda kwa wafanyabiashara wengine, basi jua kuna thamani kubwa zaidi wanayoipata kwa wale wafanyabiashara wengine ambayo kwako hawaipati.

Na kama hakuna thamani kubwa, basi hakuna utofauti kwao iwapo watakuja kwako au wataenda kwa hao wafanyabiashara wengine.

Sasa kuendesha biashara yako bila ya kujenga utofauti ambao wateja wataona thamani kubwa kwako kuliko kwa wengine ni kuendesha biashara kwa hatari kubwa.

Hatua ya kwanza na ya muhimu kabisa ya kukuwezesha kutengeneza wateja watakaoendelea kuwa kwenye biashara yako ni kutengeneza utofauti baina yako na wafanyabiashara wengine.

Hakikisha kwenye biashara yako, mteja kuna huduma anazopata, ambazo hawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote. Ni huduma hizi za kipekee ndiyo zitawafanya wateja waendelee kuwa na wewe, kwa sababu wanajua hawana pengine pa kuzifuata.

Hatua ya pili ni kutoa thamani kubwa sana inayozidi kiasi ambacho mteja analipia. Wateja wanaweza kuondoka kwako wakisema unauza ghali na kwenda kwa wafanyabiashara wengine wanaouza kwa bei rahisi. Sasa usikimbilie kupunguza bei ili kuwafanya wateja wasiondoke, badala yake kazana kuongeza thamani zaidi. Unapotoa thamani kubwa sana, ambayo kwa mwonekano ni zaidi ya kile mteja alicholipia, wateja wataendelea kuwa na wewe kwa muda mrefu.

Hatua ya tatu ni kutengeneza mahusiano bora sana na wateja wako. Wateja wanapaswa kukuchukulia wewe kama rafiki yao, kama mtu unayejali sana kuhusu maisha yao na mafanikio yao na siyo unaangalia tu kupata pesa zao. Katika hali yoyote ile, watu wanapenda kununua kutoka kwa marafiki zao, kuwa rafiki wa wateja wako na watanunua zaidi kwako.

SOMA; Mambo Matano Muhimu Kuzingatia Ili Kuimarisha Huduma Mteja Anayopata Kwenye Biashara Yako.

Hatua ya nne ni kuwafikia wateja wapya kila wakati. Kuna wakati wateja ulionao watapungua kwa sababu mbalimbali. Labda wengine wataenda mbali, wengine watakuwa hawahitaji tena huduma zako na kadhalika. Hivyo kila wakati unahitaji kuwa unawafikia wateja wapya wa biashara yako. Wateja hao wapya wape huduma bora sana na jenga nao mahusiano mazuri na watakuwa wateja wako.

Hatua ya tano ni kuweka makubaliano na mteja kabla. Kwa mfano kwenye hilo la upigaji wa picha kwenye matukio fulani, badala ya kwenda pale na kutaka watu wapige picha kwako, unaweza kuwatafuta wale watakaoshiriki tukio hilo na kuweka nao makubaliano ya kuwapiga picha nzuri sana kwao. Kama ni mahafali, kabla ya siku ya mahafali, tafuta baadhi ya wale wanaohitimu ambao watahitaji huduma ya picha, kisha ingia nao makubaliano ya kuwapiga picha, huku ukiwapa ahadi ya thamani kubwa kwao. Inapofika siku ya tukio hutakuwa na haja ya kukimbizana na kila mteja, maana tayari umeshaingia makubaliano na wateja wako utakaowapa huduma nzuri.

Hatua ya sita ni kuwakaribisha wateja wako vizuri. Unaweza kuona hicho ni kitu kidogo sana lakini kina umuhimu mkubwa sana. Usifikiri watu watakuja kununua au kupata huduma kwako kwa sababu unaonekana kuwepo kwenye biashara. Watu watakuja kwa sababu umewakaribisha na wakati mwingine kuwang’ang’aniza. Ukiona wateja wanakupita na kwenda kwa wengine, jua kule wanakoenda wamekaribishwa. Andaa salamu nzuri ya kuwakaribisha wateja wako na itumie kwa kila mteja. Kama ambavyo kondakta wa daladala anaweza kumuuliza hata abiria aliyeshuka kwenye gari lake muda huo huo, unaenda? Kwa sababu anajua anaweza kuwa amebadili mawazo na akawa mteja tena.

Zingatia hatua hizo sita muhimu na utaweza kutengeneza wateja wazuri sana kwenye biashara yako.

Kwenye eneo la pili kuhusu kufungua studio, kitu kikubwa cha kuzingatia ni kuifanya studio yako kuwa eneo litakalotoa huduma bora kabisa kwa wateja wako. Jiulize ni tatizo lipi la wateja wako unalotatua, kisha hakikisha studio yako inaweza kutatua tatizo hilo. Weka kila mteja atakachohitaji ili kupata picha bora kabisa kwake.

Nakutakia kila la kheri katika kuendesha na kukuza biashara yako kwa kutengeneza wateja wanaotegemea zaidi biashara yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog