Siku hizi kuna mbinu na njia za mkato kwenye kila kitu.

Utasikia kuna mbinu na njia ya mkato ya kupunguza uzito, kwamba unakunywa tu kidonge na uzito unapungua.

Wengine watakuambia kuna programu ya simu janja ambayo itakusaidia kufanya vitu fulani.

Na kwenye fedha na mafanikio, ndiyo kabisa kila siku kuna mtu anaibuka na mbinu mpya za kupata fedha kwa haraka na bila ya kufanya kazi.

Maisha haya ya mbinu na njia za mkato yamewapoteza wengi. Kwa sababu, kwanza mbinu hizi hazifanyi kazi, lakini kabla mtu hajaona haifanyi kazi, tayari anakuwa ameshaingia kwenye mbinu nyingine. Hivyo hawezi kukaa chini na kutathmini kama mbinu hizi zinamsaidia au la.

Rafiki, achana na mbinu na njia za mkato, chagua kufanya kitu sahihi na kifanye kwa usahihi hasa.

Chagua ni kitu gani unataka kufanya kwenye maisha yako, kisha kijue kitu hicho kwa undani, kijue hasa na jua kuna kazi inahusika mpaka uweze kukipata.

Ukishakijua vizuri na kujua kuna kazi unahitajika kufanya, weka kazi hiyo. Weka juhudi kubwa sana kwenye kufanya, na usihangaishwe kabisa na mbinu au fursa za mkato zinazojitokeza.

Mwisho wa siku, kazi bora itasimama yenyewe, huku mbinu na njia za mkato zikija na kupita.

Hata kama utaona njia ya mkato ambayo wengine wanakuambia imewasaidia sana, kama haihusishi kufanya kazi, kama haihusishi kufanya kilicho sahihi, achana nayo, itakupotezea muda wako na kukuondoa kwenye kazi sahihi kwako.

Ukishajitoa kufanikiwa, kwanza kabisa achana na mbinu za haraka na njia za mkato. Hizo ni njia za wanaoshindwa kujiliwaza na kupoteza muda. Wewe huhitaji kujiliwaza au kupoteza muda, unahitaji kuweka kazi ili upate matokeo bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha