Rafiki yangu mpendwa,
Upo usemi kwamba mafanikio ya mtu kwenye maisha ni wastani wa mafanikio ya wale watu watatu wanaomzunguka, anaotumia muda mwingi kuwa nao.
Hatuwezi kufanikiwa kuliko wale waliotuzunguka, hivyo hawa ni watu ambao tunapaswa kuwa nao makini sana.
Ukizungukwa na watu waliofanikiwa au wanaotaka kufanikiwa zaidi, utaweza kupiga hatua kama wao.
Lakini kama utazungukwa na watu waliokata tamaa na maisha yao, watu wanaofanya kwa mazoea, na wewe pia utaishi kwa mazoea.
Sasa, wengi wamekuwa wakikata tamaa kwa kuona hawana watu wazuri wa kuwazunguka na hivyo kuona hawana cha kufanya ili wafanikiwe.
Hapa ni pale mtu anapozungukwa na watu ambao hawana hata msukumo wa kufanya kitu cha tofauti. Wengi wanaona kama wameshakwama na hakuna namna yoyote kwao kupiga hatua zaidi.
Zipo njia mbili ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzitumia kujifunza kutoka kwa wengine, akaweza kufanya makubwa na kufanikiwa zaidi.
Njia ya kwanza ni kuwa na watu chanya wa mfano ambao unawafuata kwa vile wanavyoishi.
Hapa haijalishi kama watu hao wapo karibu au wapo mbali, iwe wapo hai au walishakufa.
Tunaishi kwenye zama za taarifa, ambapo ni rahisi sana kupata taarifa na maarifa yoyote ambayo mtu unayataka kuhusiana na mtu yeyote yule.
Na uzuri ni kwamba, wengi walioonja ukuu kwenye maisha yao, waliacha alama ambayo inaweza kuwasaidia wengine nao kufikia ukuu. Waliandika vitabu wao wenyewe au kuna watu waliandika vitabu kuhusu wao.
Chagua watu ambao unahamasishwa sana nao, chagua watu ambao unataka maisha yao yafike ngazi walizofika wao. Kisha jifunze kila kitu kuhusu wao na ishi misingi ya maisha ambayo wao waliishi.
Kwa njia hii utahitaji kujifunza sana hasa pale ambapo huwezi kukutana na watu hao. Kuijua misingi ambayo watu hao waliishi. Na kabla hujafanya chochote, unajiuliza kama angekuwa yule unayemfuata, angechukua hatua gani kwenye hali kama ambayo upo wewe?
Njia hii kila mtu anayetaka kufanikiwa anaweza kuitumia na akapata matokeo mazuri sana. Ni wewe kuchagua aina ya watu ambao ungependa maisha yako yafike ngazi walizofikia wao na kisha kuweka kazi.
Njia ya pili ni kuwaangalia walioshindwa kisha kufanya kinyume na walivyofanya wao.
Kama huwezi kupata watu waliofanikiwa wa kukuongoza, na kama hupati vitu vya kujifunza kupitia watu hao, ipo njia nyingine nzuri sana ya kujifunza.
Njia hiyo ni kuwaangalia wale walioshindwa, kisha kufanya kinyume kabisa na jinsi walivyofanya wao. Angalia ni makosa gani waliyafanya kwenye maisha yao na epuka kuyafanya maisha yao.
Angalia jinsi waliishi maisha yao yote, na wewe epuka kabisa kuishi aina maisha ya aina hiyo.
Mwandishi mmoja aliwahi kuandika, kama unamjua mtu ambaye aliwahi kufanikiwa huko nyuma kisha akaanguka vibaya, basi mtafute na omba kuongea naye kwa muda huku ukiwa umebeba kijitabu cha kuandika yote muhimu. Kisha muulize ilikuwaje akaanguka kutoka kwenye mafanikio?
Na mimi nakuambia, kama unamjua mtu ambaye ameishi miaka mingi lakini hakuna kikubwa alichofanya kwenye maisha yake, na muda wote amekuwa amelalamika kuhusu maisha, omba muda wa kukaa naye na jifunze kwake. Wala usimuulize kwa nini alishindwa, wewe muulize ni kwa jinsi gani ameishi maisha yake, na kama angerudi kwenye ujana sasa, ni vitu gani angefanya kwa utofauti.
Watu wengi huwa wanajibu kwa uaminifu kuhusu maisha yao, hivyo utaweza kujifunza mengi sana kuhusu maisha na mafanikio.
SOMA; Siri Muhimu Ya Mafanikio Kwenye Zama Hizi Za Mafuriko Ya Maarifa Na Taarifa.
Kwa njia hii ya pili, kila mtu anaweza kujifunza na akachukua hatua.
Kama upo kwenye ajira, angalia mtu aliyekaa kwenye ajira hiyo kwa miaka mingi na hakuna hatua amepiga, kisha angalia amekuwa anafanyaje kazi zake na epuka kufanya kazi kama yeye.
Kama upo kwenye biashara, angalia wale ambao wamekaa kwenye biashara ya aina hiyo kwa muda mrefu lakini hakuna hatua kubwa walizopiga. Kisha angalia wanaendeshaje biashara zao na epuka kuendesha biashara yako kama wao.
Rafiki yangu, hizo ndiyo njia mbili za kujifunza kutoka kwa wengine, kuangalia wale unaotaka kuwa kama wao na kujifunza jinsi wameishi maisha yao, au kuangalia wale ambao wameshindwa na kuepuka kuishi maisha kama yao. Je unashindwa hili kweli? Usiniambie tena huna watu wazuri wa kujifunza kwao, kila aliyekuzunguka kuna kitu anajaribu kukufundisha na maisha yake, jifunze na chukua hatua.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha