Mteja wa kwanza na muhimu sana kwa biashara yako, ni mtu yeyote ambaye anafanya kazi kwenye biashara yako.

Wasaidizi wako kwenye biashara, yeyote yule anayejihusisha na biashara hiyo, ni mteja wa kwanza na wa muhimu sana kwenye biashara yako.

Kwa sababu hawa ni wateja ambao wanaweza kuwakaribisha wateja wakanunua zaidi au wakawafukuza wateja wasinunue au wasirudi tena.

Hivyo unahitaji kuweka umuhimu na kipaumbele kwa wateja wako hawa muhimu.

Kwanza kabisa lazima wateja hao waamini kwenye biashara hiyo, lazima waamini kile biashara inauza ndiyo kitu muhimu kabisa kwa mteja. Kama watu hawa hawaamini hivyo, basi hata wateja hawataamini na utajikuta huuzi.

Pili lazima wajue vizuri biashara hiyo na kujua hitaji la wateja wanaokuja kwenye biashara. Wasiwe kwenye biashara halafu wakashindwa kumjibu mteja swali ambalo anataka kujua kuhusu mnachouza. Hivyo lazima uwajali kwa kuhakikisha wanajua vizuri kuhusiana na biashara yako na kila mnachouza.

Tatu na mwisho unahitaji kuwajali sana kwa kuhakikisha wanapata maslahi mazuri kulingana na uwezo wa biashara kuwalipa. Tekeleza kile ulichowaahidi, hasa kwenye malipo. Na hata kama huna uwezo wa kuwalipa kiasi kikubwa, basi kile kidogo ulichoahidi walipe kwa wakati. Pia usisahau kuwapa zawadi mbalimbali kulingana na juhudi wanazoweka kwenye biashara yako.

Sheria ni hii; kama utawajali watu wako, watawajali wateja wako na biashara itajijali yenyewe. Mteja akishajaliwa, basi na biashara imejaliwa. Wajali watu wako na biashara itajijali yenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha