Kuna baadhi ya vitu inabidi uone huruma kujifanyia kwenye maisha yako, kwa sababu kila mtu anakazana kukufanyia.

Moja ya vitu hivyo ni kukata tamaa. Watu wengi waliokuzunguka wanajaribu kukukatisha tamaa. Sasa kama na wewe mwenyewe utajikatisha tamaa, nafasi yako ya kufanikiwa itakuwa sifuri kabisa.

Unahitaji kuwa mtu pekee ambaye atasimama upande wako, ambaye ataendelea kupambana licha ya kukutana na magumu, ambaye ataendelea kuamini kwenye ndoto yako.

Kwa sababu kama wewe hutachukua nafasi hiyo, hakuna atakayeichukua na kwa hakika hutaweza kupiga hatua kubwa.

Kitu kimoja ambacho umekuwa unatumia kujikatisha nacho tamaa ni kuona hujakamilika. Pale unapokuwa na wasiwasi ndani yako, pale vitu vinapokuwa vinakinzana, pale unapoona maamuzi fulani uliyofanya ulikosea ndipo unapojikatisha tamaa na kuona huwezi kuendelea.

Unahitaji kujikubali vile ulivyo, kukubali kwamba hujakamilika, kukubali kwamba unaweza kufanya makosa mbalimbali na kwamba siyo lazima ukubaliane na kila kitu au vitu vyote viende kama unavyotaka wewe.

Lazima ukubali kwamba maisha yako hayatakuwa kama ulivyotarajia yawe wakati wote, na hakuna tatizo lolote kwenye hilo.

Jua kabisa ya kwamba, huhitaji kuanza ukiwa mkamilifu, wala huhitaji kukazana kufikia ukamilifu, bali unachohitaji ni kukazana kuwa bora zaidi kila siku kuliko ulivyokuwa jana. Ukiweza hili la kukazana kuwa bora zaidi kila siku, utaweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako na utaepuka kujikatisha tamaa wewe mwenyewe.

Acha kujikatisha tamaa wewe mwenyewe, tayari kila mtu anajaribu kufanya hivyo kwako, hivyo simamia ndoto yako na kazana kuwa bora zaidi kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha