Rafiki yangu mpendwa,

Tupo pale tulipo leo kwa sababu ya hatua tulizochukua jana, na kile tunachofanya leo ndiyo kinatengeneza kesho yetu.

Hii ina maana kwamba, baadhi ya vitu tunavyofanya leo vinaifanya kesho yetu kuwa bora zaidi au vinaivuruga kesho yetu.

Kila tunachofanya leo, tunapanda mbegu kwa ajili ya kesho, tunawekeza kwa ajili ya kesho.

Watu wamekuwa wanafanya vitu ambavyo hawajui hata vina msaada gani kwao, halafu wanashangaa pale kesho zao zinapokuwa hovyo.

Kuna uwekezaji mmoja muhimu sana ambao unaweza kuufanya kwenye maisha yako leo na ukakulipa sana kwa kesho. Uwekezaji huu unakufanya wewe kuwa bora na kuweza kupata chochote kile unachotaka.

Uwekezaji tunaozungumzia hapa ni uwekezaji unaofanya ndani yako mwenyewe. Kile unachofanya leo ili kuwa bora zaidi, kinakuwezesha kufanya makubwa zaidi kesho na kuweza kupiga hatua zaidi.

vitabu softcopy

Kadiri unavyokazana kuwa bora leo, ndivyo unavyoweza kufanya makubwa zaidi kesho. Kadiri unavyotatua changamoto unazokutana nazo leo, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya mafanikio zaidi kesho.

Ni hatua zipi unazoweza kuchukua ili kuwa bora zaidi leo kama uwekezaji kwa ajili ya kesho?

Zipo hatua nyingi, kwa chochote unachofanya ambacho kinakuacha ukiwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana, ni uwekezaji.

Lakini zipo zile hatua muhimu zaidi ambazo kila mtu anapaswa kufanya kila siku ili kuwa bora zaidi;

Moja; jifunze kitu kipya kila siku.

Hapa unahitaji kujifunza kitu kipya kila siku kwa kusoma vitabu, kusikiliza vitabu vilivyosomwa na hata kuangalia mafunzo yanayotolewa kwa njia ya video.

Kila siku unahitaji kuingiza kitu kipya kwenye akili yako, ili akili yako itanuke zaidi, uweze kufikiri sawasawa na uweze kuona yale ambayo ulikuwa huoni.

Kwa sababu wanasema macho hayawezi kuona kile ambacho akili yako haijui.

Kadiri unavyojua zaidi ndivyo fursa mbele yako zinakuwa nyingi zaidi.

Mbili; ipe akili yako mazoezi kila siku.

Pamoja na kujifunza, unahitaji kuipa akili yako mazoezi kila siku. Unahitaji kukaa chini kwa utulivu na kuipa akili yako jukumu la kuja na mawazo mbalimbali ambayo siyo lazima yawe sahihi au ya matumizi.

Unaipa akili yako zoezi la kufikiri kwa kina na kuondokana na usumbufu. Unaweza kujipa zoezi la kuandika mawazo kumi kuhusiana na kitu fulani. Pia unaweza kuandika changamoto uliyonayo na kuorodhesha njia mbalimbali za kutatua changamoto hiyo.

Kwa vyovyote vile, hakikisha akili yako inakuwa imara kwenye kufikiri kwa kina na kuja na mawazo bora kwenye hali yoyote ile.

SOMA; Karibu Kwenye Semina Ya KISIMA CHA MAARIFA 2018; Mafanikio, Biashara Na Uhuru Wa Kifedha.

Tatu; tengeneza mtandao wa mamenta.

Unahitaji kuwa na menta kwenye kila eneo la maisha yako unalotaka kufanikiwa. Menta ni mtu ambaye unamwangalia na ungependa kupiga hatua kama ambazo amepiga yeye. Mamenta wanakufundisha mambo ambayo ulikuwa hujui na kukusaidia kuvuka changamoto ambazo huenda unaona ni kubwa sana kwako.

Kwa kuwa na menta, unaepuka kufanya makosa ambayo yatakuchelewesha, pia unapata ushauri ambao unakusaidia kupiga hatua kubwa zaidi.

Nne; fanya kitu cha kuboresha afya yako kila siku.

Kama afya yako ya mwili itakuwa mbovu, hutaweza kupiga hatua kama ambavyo unatarajia kupiga. Na njia bora ya kuimarisha afya yako ni kujikinga na magonjwa mbalimbali ambayo yanawarudisha watu wengi nyuma.

Kula kwa afya, fanya mazoezi na pata muda wa kupumzika. Hivi ni vitu vitatu ambavyo ukivifanya kwa usahihi afya yako itakuwa imara na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Hizo ndiyo hatua muhimu sana kwako rafiki yangu kuchukua katika kufanya uwekezaji bora sana kwako, ambao utakuwa uwekezaji bora kwenye maisha yako.

Nikutakie kila la kheri katika kukazana kuwa bora zaidi kila siku.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji