Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri sana kwa kila mmoja wetu kwenda kupiga hatua zaidi kwenye maisha yake,
Leo, kwenda kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa jana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HAKI YA KUZALIWA NA HAKI YA KUPATA…
Nimekuwa nakuambia MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA, na hili limekuwa linawapa watu faraja kwamba wanayp haki ya kufanikiwa, na kujisikia vizuri pia.
Lakini sasa wamekuwa wanaishia hapo, wakijiambia mafanikio ni haki yangu, ipo siku yangu na mimi nitafanikiwa.
Halafu wanaendelea na maisha ya kawaida, wanafanya kazi kawaida, wanachezea muda kwa kuangalia kila habari, kuzurura kwenye kila mtandao na hata kulewa.
Kitu ambacho nimekuwa simalizii kwenye sentensi hiyo ni kwamba HUNA HAKI YA KUPATA MAFANIKIO. Na hili najua halitakupa faraja, halitafanya ujisikie vizuri, lakini pia halitafanya uendelee kujidanganya kuhusu mafanikio yako.
Sasa tukiweka hayo mawili kwa pamoja tunapata kauli hii muhimu sana ambayo unapaswa kuitumia kwa mafanikio yako. MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA, LAKINI HUNA HAKI YA KUPATA MAFANIKIO.
Hakuna mtu yeyote atakayekupa wewe mafanikio, siyo ndugu, siyo wazazi, siyo serikali, siyo marafiki.
Mafanikio hayatakuja kirahisi kwa kuendelea kuishi kama ulivyozoea kuishi, kama ambavyo kila mtu anaishi.
Hutafanikiwa kwa kutaka kukubaliana na kila mtu, kutaka kumfurahisha kila mtu.
Huna haki ya kupata mafanikio kwa sababu mafanikio yanapiganiwa, mafanikio yanapatikana kwa wale wanaojitoa hasa, wanaokuwa tayari kuumia na kuendelea bila ya kukata tamaa.
Hivyo usifanye makosa ya kujidanganya kwamba ipo siku yako utafanikiwa, angalia kwanza hatua unazochukua, kama ni za kawaida, kama unaendesha maisha yako kama wengine wanavyoendesha, kama kila mtu anakubaliana na wewe, kama unaonekana ni mtu wa kawaida, utapata kila unachotaka, lakink siyo mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa yametengwa kwa wale wachache ambao wana ngozi ngumu, wanaoweza kuvumilia na kuvuka kila aina ya kikwazo bila ya kukata tamaa.
Swali ni je wewe ni mmoja wa hao wenye ngozi ngumu na wanaopambana ili kufanikiwa?
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi uhalisia wa maisha yako na siyo kujidanganya.
#Fanya#HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha