Rafiki yangu mpendwa,
Ubinafsi ni kitu ambacho kimekuwa kinapewa sura mbaya sana kwenye maisha yetu ya kila siku.
Ubinafsi umekuwa unaonekana ni kitu kibaya, umekuwa unaonekana ni tamaa na kutokuwajali wengine.
Tumekuwa tunasisitizwa kuwa na upendo wa mshumaa, kuwamulikia wenzetu wakati sisi wenyewe tunaisha.
Na yote hayo ni kweli kabisa, kwamba hatuwezi kuendelea kama jamii kama kila mtu atakuwa mbinafsi.
Kama kila mtu atataka apate anachotaka, bila ya kujali wengine wanapata nini, jamii haiwezi kwenda, itaanguka.
Hivyo tunapaswa kuwafikiria wengine kwenye kila maamuzi tunayofanya, na kujiuliza je maamuzi hayo yanaathiri vipi maisha yao.
Lakini pia hatuhitaji kutokuwa wabinafsi kabisa. Kwa sababu kuchagua kutokuwa mbinafsi kabisa kwenye maisha yako ni kujizuia wewe mwenyewe kufanikiwa.
Kama kwenye kila jambo unalotaka kufanya kwenye maisha yako utaangalia kwanza wengine, au kama utamsikiliza kila mtu kwenye kila unalotaka kufanya, kwa hakika hakuna hatua utakayoweza kupiga kwenye maisha yako.
Hivyo ili kufanikiwa, kuna kiwango cha ubinafsi ambacho lazima kila mmoja wetu awe nacho.
Tunapoambiwa tusiwe wabinafsi, inaonekana kama kila aina ya ubinafsi ni mbaya. Lakini ukweli ni kwamba, zipo aina za ubinafsi ambazo ni muhimu kwa mafanikio ya kila mmoja wetu.
Yafuatayo ni maeneo muhimu sana kwako kuwa mbinafsi ili uweze kufanikiwa.
Moja; ubinafsi kwenye afya yako.
Huwezi kuwasaidia wengine kama afya yako itakuwa kwenye matatizo, hivyo kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako kinapaswa kuwa afya yako. Unahitaji kwenda hatua ya ziada kuhakikisha unakuwa na afya bora ili uweze kuwasaidia wengine pia.
Haijalishi unataka kuwasaidia wengine kiasi gani, kama afya yako haipo vizuri, hutaweza kumsaidia yeyote na sana sana utakuwa mzigo kwa wengine.
Tenga muda wa kuweza kula vizuri, kufanya mazoezi na kupumzika ili mwili wako uwe imara kwa majukumu yako. Na haya yanapaswa kuwa kipaumbele kikubwa kwako.
Mbili; ubinafsi kwenye muda wako.
Hebu angalia, una masaa 24 tu kwenye siku yako, huwezi kupata hata dakika moja ya ziada. Ukitoa muda unaolala, unaokula na kufanya mengine muhimu ambayo ni nje ya kazi, utabaki labda na masaa 14 kwa siku. Sasa swali linakuja unafanya nini kwenye masaa hayo 14?
Unahitaji kuwa na ubinafsi kwenye muda wako kama kweli unataka kupiga hatua kwenye maisha. Kwa sababu muda wako una ukomo, na hakuna anayeweza kuzalisha muda zaidi.
Lazima upime sana kila unachotaka kufanya, na uone kama ndiyo kitu muhimu zaidi kwako kufanya kwa muda ulionao. Kama siyo kitu muhimu basi usifanye, hata kama kila mtu anafanya, hata kama kila mtu anategemea.
Tumia muda wako vizuri kwa sababu hutapata zaidi.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Own The Day, Own Your Life (Imiliki Siku Uyamiliki Maisha Yako).
Tatu; Ubinafsi kwenye fedha zako.
Watu wengi hufikiri kuwa na roho nzuri ni kuwapa watu fedha kwa kadiri wanavyotaka, hata kama hawana umuhimu mkubwa. Hivyo watu wanapopata fedha, wanashangaa hawajui zinaishia wapi. Wakati mwingine mtu anapokuwa na fedha ndiyo kila anayemzunguka anakuwa na dharura na kuhitaji fedha hizo. Lakini fedha zikiisha hakuna tena anayemsumbua.
Unahitaji kuwa na ubinafsi kwenye fedha zako. Na siyo ubinafsi kwamba usiwajali kabisa wengine, bali uweke kipaumbele kikubwa kwenye matumizi ya fedha zako, iwe ni kuzalisha zaidi na siyo kutumia zaidi. Maana fedha ukishaitumia umeipoteza, lakini ukiiwekeza unaizalisha zaidi.
Linapokuja swala la fedha, kauli yangu huwa ni moja; KILA MTU NA APENDE FEDHA ZAKE. Hakuna atakayejali kuhusu fedha zako kama wewe mwenyewe hutaweza kuzijali.
Usikimbilie kuwapa watu fedha kwa sababu tu wamekuambia wana wazo bora sana ila wamekwama fedha. Taka kwanza kujua wazo hilo bora ni lipi na utashangazwa jinsi ambavyo mtu anataka kutumia fedha zako kufanya kitu kilicho hatari na kisicho na matumaini ya manufaa mazuri.
Penda fedha zako kwa kuzisimamia vizuri na kuzifuatilia pia.
Nne; ubinafsi kwenye uhuru wako.
Usikubali kupoteza uhuru wako kwa mtu yeyote yule. Kama kuna kitu muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako fanya. Na kama kuna kitu hutaki kufanya usifanye.
Hakuna utumwa mkubwa kwenye maisha kama kufanya kitu ili kuwafurahisha wengine. Maana wewe utafikiri unawafurahisha, lakini wao hata hawajali.
Jifunze kusema HAPANA pale ambapo hutaki kufanya kitu fulani ambacho watu wanataka ufanye lakini siyo muhimu kwako. Ndiyo ni ubinafsi, lakini ni muhimu sana kwa mafanikio yako.
Tano; ubinafsi kwenye akili na umakini wako.
Usiruhusu kila mtu aje atupe uchafu wake kwenye akili na umakini wako. Hasa kwa habari hasi, umbeya, majungu na kufuatilia maisha ya wengine.
Mara zote ifanye akili yako kufikiri mambo chanya na umakini wako kuwa kwenye yale ambayo ni muhimu kwako.
Hivyo kuwa mbinafsi kwa kuepuka kabisa habari zote hasi, kuacha kupoteza muda wako kwenye mitandao ya kijamii isiyokuwa na mchango kwenye mafanikio yako.
Rafiki, kama wanavyosema kwenye ndege, vaa kwanza vifaa vya kukuokoa wewe kabla hujataka kumwokoa mtu mwingine, kwenye maisha, hakikisha kwanza wewe uko vizuri kabla hujataka kuwasaidia wengine. Hivyo unahitaji sana kuwa na ubinafsi kwenye maeneo yale muhimu kwenye maisha yako, kwa kuwa na mipango unayofanyia kazi bila ya kujali wengine wanasema au kufanya nini.
Ubinafsi ni mzuri pale unapokuandaa kuweza kuwasaidia wengi zaidi. Na kusema ndiyo kwa kila kitu siyo kutokuwa mbinafsi, bali ni kutaka kumfurahisha kila mtu na unaweza kuwa ubinafsi mbaya sana.
Usijisikie vibaya pale unapoweka vipaumbele ambavyo vinakutaka useme hapana kwa mambo yasiyo muhimu zaidi kwako. Ubinafsi unaofanya maisha yako kuwa bora ni ubinafsi wenye manufaa kwa wengine pia.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha