Rafiki yangu mpendwa,

Kupitia utafiti nilioufanya kwenye maandalizi ya semina ya TABIA ZA KITAJIRI, nimejifunza ya kwamba kuna uhusiano wa karibu sana kati ya mtazamo wa mtu na mafanikio yake kimaisha.

Wale watu ambao wana mtazamo chanya, mtazamo wa inawezekana, ndiyo ambao wana mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Lakini wale wenye mtazamo hasi, mtazamo wa kushindwa na haiwezekani, hakuna hatua kubwa waliyopiga kwenye maisha yao.

Hii ina maana kwamba kama wewe rafiki yangu utatengeneza mtazamo bora kwako, utaweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. Pia kadiri mtazamo wako unavyokuwa bora, ndivyo kipato chako kinavyoongezeka pia.

Leo nimekuandalia hatua sana za kuweza kujitengenezea mtazamo bora wa maisha yako na kuweza kuongeza kipato chako. Karibu ujifunze hatua hizi na uzifanyie kazi ili maisha yako yaweze kuwa bora.

MIMI NI MSHINDI

Kabla sijaingia kwenye hatua hizi nikupe angalizo, zinaweza zisikupendeze, kwa sababu kuna vitu unapenda kufanya itabidi usivifanye. Hivyo kama hutaki kujisikia vibaya nakushauri usiendelee kusoma. Na kama utaendelea kusoma basi usifike mwisho na kusema baadhi ya vitu si sahihi kwa sababu unavitumia vizuri. Chukua kila unachojifunza hapa na kifanyie kazi.

Hatua ya kwanza; EPUKA MAGAZETI, REDIO NA TELEVISHENI.

Vyombo hivyo vya habari, huwa vinaingiza kipato kupitia matangazo na ili viweze kupata matangazo vinahitaji kuwasisimua watu ili waendelee kuvifuatilia. Na njia bora ya kuwasisimua watu ni kuwa na habari na matukio hasi. Fungulia chombo chochote cha habari, hasa wakati wa habari na lazima utakutana na habari hasi, watu kuuana, ajali, wizi na mengineyo.

Huhitaji habari hizi hasi kwenye maisha yako, kwa sababu hazina msaada wowote kwako. Hivyo epuka sana vyombo hivyo vya habari, hasa wakati wa habari.

Kuianza siku yako kwa habari hasi ni kitu ambacho kitakufanya ushindwe kufanya makubwa kwenye siku hiyo. Habari hasi unazoanza nazo zinakufanya ushindwe kuona upande chanya wa vitu vingi unavyokutana navyo. Kila unachokutana nacho utaona ni kibaya au kimefanywa vibaya. Ndiyo maana unapaswa kuepuka sana habari hasi.

Hatua ya pili; EPUKA MITANDAO YA KIJAMII.

Mitandao ya kijamii ni mashine mpya ya kuzalisha na kusambaza habari hasi. Mitandao hii imekuwa ni sehemu ambayo kila mtu anaweza kusema chochote anachotaka kusema kwa wakati wowote anaotaka kusema. Faida inayosemwa kwamba mitandao hii inayo, haizidi hasara yake.

Hivyo kama unataka kuwa na mtazamo chanya, mtazamo bora wa mafanikio, epuka sana mitandao ya kijamii. Mitandao hii inasambaza mtazamo hasi kwa urahisi sana, inakufanya upoteze muda wako kufuatilia vitu ambavyo hata siyo halisi.

Watu wengi wanaigiza maisha ambayo wanayaweka kwenye mitandao hiyo. Hivyo unaweza kujikuta unakazana kufuatilia kile wengine wanachoweka, kumbe hata siyo uhalisia.

Mitandao ya kijamii imekuwa hatari kuliko hata vyombo vya kawaida vya habari, kwa sababu tunaweza kuifikia kiurahisi na inaambatana na sisi kwa masaa 24 ya siku, siku saba za juma kupitia simu tunazobeba na hata kulala nazo.

SOMA; Ubinafsi Ni Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako Makubwa, Soma Hapakujua Maeneo Ya Kuweka Ubinafsi Kwenye Maisha Yako.

Hatua ya tatu; EPUKA KILEVI CHA AINA YOYOTE ILE.

Pombe, sigara, madawa ya kulevya na aina nyingine za vilevi vinakwenda kuharibu akili yako na hata fikra zako. Hivi ni vitu unavyopaswa kuviepuka kabisa kama unataka kutumia akili yako vizuri na kujijengea mtazamo chanya na bora kwa maisha yako.

Tatizo la vilevi vinakupumbaza, usione uhalisia, na kama unataka mafanikio makubwa, lazima uweze kuona uhalisia kwa muda wote. Na hapo bado madhara ya kiafya ya vilevi hivi. Kwa kifupi kaa mbali na aina yoyote ya kilevi.

Hatua ya nne; KAA MBALI NA WATU WA HAIWEZEKANI.

Kuna watu ambao kila ukienda kwao na wazo la kufanya kitu cha tofauti, hata kabla hawajakusikiliza unapanga kufanyaje, tayari wana jibu kwamba haiwezekani. Hawa ni watu unaopaswa kuwaepuka sana, hata kama ni wa karibu.

Watu ambao kila kitu kwao hakiwezekani, kadiri unavyokaa nao wanakuaminisha na kukubadilisha, mwishowe unakubaliana nao kwamba haiwezekani.

Usijidanganye kwamba utaweza kuwashinda watu hawa, au utashirikiana nao kwa yale ambayo yanawezekana na kutokuwasikiliza kwa yale wanayosema hayawezekani, ukishakaa karibu na watu hawa, jua kila kitu hakitawezekana kwako. Dawa pekee ni kuwaepuka.

Hatua ya tano; KILA ANAYEHUSIKA NA MAISHA YAKO AKAE UPANDE WAKO.

Kwenye vita au mapambano kuna kauli kwamba kama haupo upande wetu basi wewe ni adui yetu. Hivyo kila anayehusika na maisha yako, anapaswa kuwa upande wako. Anapaswa kujua ni nini unafanya na wapi unataka kufika, kisha ajue anahusikaje kukusaidia kufika pale. Kama mtu atakataa kuwa upande wako, basi huyo amechagua kuwa adui kwako na hupaswi kumpa nafasi.

SOMA; Vitu Vitatu Pekee Unavyoweza Kuvidhibiti Kwenye Maisha Yako Na Vikakuletea Mafanikio Makubwa Sana.

Hatua ya sita; CHUKULIA MAZUNGUMZO HASI KAMA UCHAFU.

Mtu akija nyumbani kwako, akiwa na mfuko wenye uchafu kisha akaubwaga sebuleni kwako na kuondoka, hutamwelewa. Utagombana naye, utamsema kwa kila mtu na hutamwonea aibu. Lakini akaja mtu nyumbani kwako, ukamkaribisha sebuleni kwako na akaanza kukupa habari hasi za namba ambavyo mambo ni magumu na hayawezekani, utamsikiliza na kumvumilia.

Hakuna tofauti ya anayemwaga uchafu sebuleni kwako na anayekuletea habari hasi, vyote ni uchafu na vipe thamani hiyo. Usikubali kamwe kupokea habari yoyote hasi, chagua kuwa kiziwi kabisa pale mtu anapoanza kuleta mazungumzo hasi, na usione aibu kumwambia mtu kwama hupendezwi na mazungumzo hayo hasi.

Hatua ya saba; TENGENA DAYATI WA KUEPUKA MTAZAMO HASI.

Huwa tumezoea kutengeneza dayati za vyakula kwa kuepuka vyakula fulani na kuongeza vyakula ambavyo ni bora. Sasa unaweza kutumia dhana hiyo kwenye kuepuka mtazamo hasi kwenye maisha yako. Unachofanya ni kuhakikisha siku zima inapita bila ya kusikiliza habari hasi, kufikiri mawazo hasi au kufanya kitu hasi. Kama ikitokea umepata wazo lolote hasi au kufanya kitu hasi, basi unafuta na kuanza tena upya. Lengo ni mpaka uweze kupitisha masaa 24 bila ya kujihusisha na chochote hasi.

Fanya dayati hii na utaona jinsi gani habari na fikra hasi zilivyokita mizizi ndani yako, na ukiweza kung’oa mizizi hiyo, utaweza kufikiri kwa usahihi na kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Rafiki, fuata hatua hizo saba ili kuhakikisha unatawala fikra zako na ukishatawala fikra zako, matendo yako yatakuwa bora na hakuna kitakachokushinda katika kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge