Kuna watu wamekuwa wanaanzisha biashara, mwanzoni inaonekana kuwa na mafanikio makubwa, lakini haichukui muda inashindwa au hata kufa kabisa.
Kinachotokea ni kwamba mtu anakuwa ameiona fursa, na anakuja na wazo la biashara ambalo linatoa suluhisho kwenye changamoto au uhitaji fulani. Basi wazo hilo linakuwa la kipekee na mafanikio yanaanza kuonekana.
Sasa mtu anapopata mafanikio haya ya awali, badala ya kuendelea kuweka nguvu zaidi ili kukuza biashara yake, anaanza kutawanya nguvu kwenye mambo yasiyo muhimu.
Anaanza kufikiri ameshakuwa mjanja wa biashara, hivyo anaanza kuingia kwenye biashara nyingine wakati ile bado haijaweza kusimama vizuri yenyewe. Anaanza kuwasikiliza wanaokuja na ushauri na mawazo ya vitu gani anaweza kufanya na yeye anaanza kufanya.
Hakuna kitu hatari kwenye biashara kama mafanikio ya haraka, maana huwa yanawapumbaza wengi, yanawafanya wasione uhalisia na kufikiri kwa kuweza biashara moja basi wanaweza kila biashara.
Hakuna ubaya wowote kutaka kuwa kwenye biashara zaidi ya moja, na kila mtu anapaswa kuwa na biashara zaidi ya moja, lakini mwanzoni mwa biashara, unahitaji kuweka nguvu zako zote kwenye biashara mpaka pale itakaposimama.
Usitawanye nguvu zako mwanzoni mwa biashara, badala yake weka muda wako, nguvu zako na rasilimali zote ulizonazo kwenye kukuza biashara hiyo. Hata kama kuna fursa nyingine nzuri kiasi gani unazoona kama zinakupita, acha tu zikupite, lakini usiyumbe kutoka kwenye biashara yako.
Unapokusanya nguvu zako zote eneo moja, unaimarisha, lakini unapotawanya nguvu zako, hasa mwanzoni unabaki kuwa dhaifu.
Angalia sana mafanikio ya awali ya biashara yako yasiwe sumu kwenye ukuaji zaidi wa biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,