Rafiki yangu mpendwa,

Kama uliona juma namba 33 tuliloanza lilikuwa refu, naamini unaona sasa hakuna urefu tena, maana juma limemalizika.

Lakini pamoja na kumalizika kwa juma hili, kuna alama mbili kuu zitabaki kwenye maisha yako yote.

Alama ya kwanza ni yale uliyojifunza kwenye juma hili, kupitia kusoma, kusikiliza na hata kuangalia. Yale uliyojifunza juma hili na ukasema kweli hili sikujua, au kweli hili ni muhimu, yataendelea kuwa na wewe maisha yako yote.

Alama ya pili ni hatua ulizochukua, hatua yoyote uliyochukua wiki hii, bila ya kujali matokeo uliyopata, inakwenda kuacha alama ya kudumu kwenye maisha yako. Kama matokeo ni mazuri utaona pale ulipotoka na kama utakuwa umeshindwa, utaondoka na somo utakalotumia maisha yako yote.

Karibu kwenye tano za juma hili, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kujifunza na kuweza kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Kumbuka msingi muhimu; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MATOKEO MAKUBWA. Hivyo jifunze na chukua hatua, na hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.

NETWORK MARKETING

Karibu kwenye dozi ya juma hili, ujipimie kiasi chako na uchukue hatua ili uweze kufanikiwa zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; MILIONI ZAKO 100 ZA KWANZA.

Nikiwa kwenye mtandao wa youtube nikiangalia baadhi ya mafunzo, nilipendekezewa video iliyoandikwa I RATHER BE DEAD THAN POOR, ikimaanisha NI BORA NIFE KULIKO KUWA MASIKINI. Hilo jina tu lilinipa hamasa ya kufungua na kuangalia nani mwenye uthubutu wa kuongea maneno makali kiasi hicho, ambayo nakubaliana nayo kwa silimia 100.

Na hapo ndipo nilipokutana na mtu anayeitwa Dan Pena, kocha wa biashara ambaye anaendesha semina zinazoitwa QUANTUM LEAP ADVANTAGE (QLA). Hawa ni wale watu ambao unajiuliza mbona kama ulichelewa sana kuwajua, kwa sababu kila kitu anachoongea au kufundisha unaona ni ukweli hasa, ambao watu wanapaswa kujua lakini hawaambiwi.

Dan Pena anaeleza kwamba mambo mengi ambayo watu wanafundishwa kwenye vitabu na semina za mafanikio ni ya kuwabembeleza. Watu hawaambiwi ule ukweli hasa, kwamba mafanikio siyo lele mama, na mafanikio makubwa siyo kwa kila mtu.

Dan anatumia lugha kali sana kwenye mafundisho yake kiasi kwamba kama moyo wako ni mwepesi, huwezi kuendelea kumsikiliza wala kumsoma. Kwa sababu anatumia ile lugha yenyewe na hakufichi chochote. Mfano kwenye baadhi ya semina zake anawaambia watu ni walaini na wepesi sana na kwa mwenendo wao hawawezi kufanikiwa.

Mtu anaenda kwenye semina aliyolipia fedha nyingi, lakini anakatisha na kuondoka siku ya kwanza. Wengine wanaishia kulia machozi kwa namna wanavyoelezwa ukweli.

Semina zake ni za bei ya juu na anawachuja watu wachache sana. Semina zake ni za siku saba na mtu analipia ada ya Euro elfu 10 sawa na fedha za kitanzania milioni 30. Hebu fikiria, unaweza kulipia semina ya siku saba milioni 30 na kwenye semina hiyo unaishia kwenda kugombezwa kama mtoto mdogo? Maana anagombeza kweli.

Sasa Dan amekuwa anaitwa THE 50 BILLION DOLLAR MAN, kwa sababu thamani ya wote aliowafundisha ni zaidi ya dola bilioni 50, zaidi ya trilioni 100 za kitanzania. Unaweza kuona kwa nini watu wapo tayari kulipa fedha nyingi, ili wakagombezwe na kulazimishwa kufanya hasa ili wafanikiwe.

Baada ya kumjua Dan Pena, nilitafuta vitabu vyake, na katika miaka yote 25 ambayo amekuwa anaendesha semina zake kila mwaka, ameandika vitabu vitatu pekee.

Moja ya vitabu hivyo ni YOUR FIRST 100 MILLION, nilianza kusoma kitabu hiki mara moja. Naweza kusema ni moja ya vitabu muhimu sana ambavyo kila mfanyabiashara anapaswa kukisoma. Ndani ya kitabu hichi, Dan ameeleza jinsi ya kuanza biashara hata kama huna kitu na kuweza kuikuza kufikia mamilioni ya dola.

Ametumia mfano wake ambapo alianza biashara kwa dola 820 na baada ya miaka nane biashara ikawa na thamani za zaidi ya dola milioni 450.

Nilitaka nichambue kitabu hiki, lakini kila mstari niliokuwa nasoma ni madini matupu. Mwishowe nikaona unaweza kuwa kama unatafsiri kitabu kizima, maana hakuna cha kuacha.

Ni kitabu ambacho kila anayetaka mafanikio makubwa sana, mwenye ngozi ngumu na asiyependa kubembelezwa anapaswa kukisoma. Lakini kama unapenda kujisikia vizuri, kama unataka kuwa na maisha ya kawaida, usionekane wa ajabu au wa tofauti, kama unapenda kuambiwa usijali utafanikiwa tu, ukisoma kitabu hiki utajisikia vibaya sana, na huenda utakata tamaa kabisa.

Sasa rafiki yangu, sitakuacha hivi hivi, bali nitakushirikisha yale muhimu sana kwenye kuanzisha na kukuza biashara yako ambayo Dan ametushirikisha kwenye kitabu chake.

  1. Mafanikio makubwa siyo kwa watu laini laini. Dan anasema dunia ya sasa watu wamekuwa laini sana. Wanataka mafanikio makubwa na wakati huo huo wanataka wamfurahishe kila mtu kwenye maisha. Hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea kwa namna yoyote ile. Na Dan anasema watu wanahitaji kuacha kujidanganya. Anasema kwenye mafanikio makubwa hakuna urafiki, na anasisitiza kabisa, kama unatafuta rafiki nunua mbwa, maana hao ndiyo rafiki wazuri, wengine mtasumbuana sana inapokuja kwenye mafanikio makubwa. Dan anasema kuna wakati aliwahi kumfukuza rafiki yake ambaye walianza naye biashara, kwa sababu alikuwa ameanza kuzoea biashara, haweki tena juhudi na biashara ikaanza kushuka.
  2. Kile ambacho kimezoeleka kufanyika ndiyo kifo cha mafanikio. Dan anatuambia, kama unafanya kile ambacho kila mtu anategemea ufanye, kwa sababu ndiyo mazoea na ambavyo wengine wote wamekuwa wanafanya, umeshayazika mafanikio yako. Dan anasema mafanikio makubwa yanahitaji wewe kuanzisha njia mpya, njia ambayo haijawahi kuwepo na wala haina mazoea. Anasema watu wote wanaoshindwa wanafanya vitu vinavyofanana, lakini wanaofanikiwa wanafanya vitu vya tofauti. Hivyo vitu kama masaa ya kufanya kazi, namna unavyoendesha biashara yako na hata maisha yako haipaswi kuwa kwa mazoea na wengine wanavyofanya, bali kwa mahitaji ya maisha yako kwa wakati huo.
  3. Unahitaji kutengeneza mwonekano wa mafanikio ili uweze kufanikiwa. Dan anasema mtu anapokutana na wewe kwa mara ya kwanza, anakuhukumu kwa mwonekano wako na hutaweza kumbadili tena kwa maisha yake yote. Kama kwa mwonekano wako unachukuliwa kama mtu wa bei rahisi, watu watakupa bei hiyo hiyo. Na kama mwonekano wako unaonekana mtu wa bei ghali na unayejiamini, watu watakupa kile unachotaka. Na katika kusisitiza hilo, kila mshiriki wa semina za Dan lazima avae suti. LAZIMA. Sijui unaelewa hapo, unahudhuria semina ya bei ghali, na bado unapangiwa nini utavaa. Unavaa suti, yenye mwonekano wa mtu wa bei ghali na anayejiamini. Mwonekano wako ni muhimu sana kwa mafanikio yako, usiuchukulie kirahisi.
  4. Tengeneza timu yako ya mafanikio makubwa. Dan anatuambia, mafanikio ya biashara yanatokana na timu inayoendesha biashara hiyo. Dana anasema, unapoendesha biashara unayotaka ifanikiwe sana, kwenye timu yako ya biashara, lazima uwe na wahasibu, wanasheria na wataalamu wengine wanaohusika na biashara yako. Na anasema watu hawa wawe wenye uelewa mkubwa sana kuhusu taaluma zao hizo.
  5. Mpango usio na mbadala. Dan anashangaa sana kwamba kuna watu huwa wanaweka mipango mbadala, kwamba mpango huu ukishindwa basi ataenda na mpango mwingine. Dan anasema, mafanikio makubwa hayana mbadala, ni mtu unayafikia au unakufa ukiyafikia. Hivyo unahitaji kutengeneza mpango usio na mbadala, mpango ambao hata ukishindwa huachi wala kubadilika, bali unajifunza na kusonga mbele zaidi.
  6. Kupata fedha kwa ajili ya kukuza biashara yako. Dan anatuambia kwamba, kuna njia moja tu ya benki kupata faida, na njia hiyo ni kupitia kukopesha. Benki hazipati faida kwa kutunza fedha za watu, bali zinapata faida kwa kukopesha watu fedha hizo na walete faida. Hivyo kama unasema huna njia za kupata fedha za kukuza biashara yako, inabidi uweze kudhibitisha kwamba unaishi eneo ambalo halina benki yoyote ile. Lakini kama benki ipo, jua kabisa meneja wa benki hiyo anatamani sana kutoa mikopo ili apate faida, lakini anahitaji pia mikopo hiyo iwe salama, yaani iweze kurudi. Hivyo ni wajibu wako wewe kutengeneza mazingira na mahusiano mazuri na mabenki kiasi kwamba unaweza kupata fedha za kukuza biashara yako. kwenye kitabu Dan ameshirikisha njia mbalimbali za kufanya hivyo, lakini kubwa sana ni kujenga mahusiano mazuri ya kibiashara na watu wa mabenki.
  7. Siri ya biashara kukua kwa kasi kubwa ni kununua biashara nyingine. Dan anatuambia kwamba ili biashara iweze kukua zaidi, inahitaji kuangalia biashara zinazoendana na biashara hiyo na kuzinunua. Dan anatuambia biashara nyingi zinaendeshwa hivyo na kwa hasara, sasa wewe ukishakuwa na mfumo mzuri wa kuendesha biashara zako, unaweza kununua biashara ambayo haiendi vizuri, ukaisuka vizuri na baadaye kuiuza au hata kuendelea nayo.

Yapo mengi sana ambayo Dan anatushirikisha kwenye kitabu hiki, ambayo yanakufanya mtu ujifunze na kusema, kumbe. Pata muda usome kitabu hiki, kitakusaidia sana, hasa kama upo tayari kwa mafanikio makubwa sana. Na kwa tahadhari tu, mambo anayofundisha Dan ni mazito na yanaweza kugharimu mtu maisha yake. Kwa mfano anatuambia mmoja wa washirika wake, alikufa mwezi mmoja baada ya kuwa wameuza biashara yao ambayo iliwagharimu sana muda na nguvu kuweza kuiuza kwa mafanikio.

Mafanikio makubwa siyo lele mama, lakini pia yanawezekana, iwapo mtu utajitoa sana.

#2 MAKALA YA WIKI; UWEKEZAJI MUHIMU SANA KWENYE MAISHA YAKO.

Watu wengi wamekuwa wanauliza sana kuhusu aina mbalimbali za fursa na biashara ambazo wanakuwa wameshirikisha kama ni sahihi kwao kufanya.

Na siku hizi kuna fursa za kila aina, kuanzia CRYTPTOCURENCY mpaka FOREX, kuanzia NETWORK MARKETING mpaka KILIMO BIASHARA.

Na katika kushauri hayo yote, nimekuwa nasema kitu hichi kimoja, kabla hujatoa fedha yako kuwekeza popote, nunua kwanza maarifa na wekeza ndani yako.

Fursa nyingi unazopigiwa kelele kwamba zinakupita siyo sahihi kwako, sasa huwezi kujua kama huna maarifa sahihi. Ndiyo maana nimekuwa nakusisitiza sana, usiweke fedha zako sehemu usiyoijua, labda kama hupendi fedha hizo.

Juma hili nilikuandikia makala kuhusu uwekezaji muhimu sana kufanya kwenye maisha yako, unaweza kusoma makala hiyo hapa; Huu Ndiyo Uwekezaji Bora Kabisa Unaoweza Kufanya Kwenye Maisha Yako, Ambao Utakulipa Sana.

Pia kuna makala nyingine nyingi za kila siku kwa juma zima kwenye AMKA MTANZANIA, tembelea na usome makala hizo mpya na nzuri.

#3 TUONGEE PESA; UMASIKINI HAUNA URAFIKI.

Hivi umewahi kugundua kwamba ukiwa na fedha unakuwa na marafiki wengi kuliko ukiwa huna fedha. Sasa wapo watu wanaosema kwamba marafiki ni wanafiki, kwamba watakupenda ukiwa na fedha lakini ukiwa huna wanakutenga.

Kwanza niseme kitu kimoja, wewe mwenyewe ukijua huna fedha unaanza kujistukia, yale maeneo ulikuwa unakutana na marafiki zako unakuwa huendi tena, wakikutafuta unawakwepa, mwishowe unabaki mwenyewe, halafu unawalaumu wao kwamba wamekutenga.

Rafiki yangu, umasikini hauna urafiki, wewe mwenyewe utajichukia ukiwa huna fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu kwako.

Hivyo kwanza kabisa wapende sana wale marafiki wanaokupenda ukiwa na fedha, kwa sababu wanakutakia mema, hata kama ni kwa sababu wanategemea mtumie fedha hizo kwa pamoja.

Na pili, pata fedha rafiki, usianze kulalamika sijui nani kasema nini kwa sababu huna fedha. Hayo yote hayatakuwa na maana kama huna fedha. Maana kama huna fedha, hata kama watu watakupa maneno ya faraja kiasi gani, jua mwisho wa siku hutakula faraja.

Pata fedha kwa sababu umasikini hauna urafiki, na unaumiza, na unashusha morali wako, na utakufanya usijiamini, na mwishowe utapelekea uanze kuwashuku wengine, hasa pale unapokuwa huwezi kuwa nao tena pamoja.

Dawa ya yote ni pata fedha na endesha maisha yako kwa namna ambayo ni muhimu kwako.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; SEHEMU PEKEE TUNAYOWEZA KUONANA.

Kila siku nashukuru sana kwa namna huduma hii ninayotoa ya mafunzo na hamasa inavyowafikia watu wengi na wapya. Wapo watu wengi wamekuwa wakiniandikia email na hata jumbe mbalimbali wakishukuru namna elimu ninayotoa inawasaidia, na mimi nawashukuru sana kwa kujifunza.

Ila sasa karibu kila mmoja wa watu hao amekuwa anakuja na ombi ambalo kwa upande wangu linakuwa gumu sana kutekeleza. Wengi wanapenda tukutane, niwashauri zaidi niwape ushauri na mwongozo kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yao. Kitu ambacho kwa upande wangu ni kigumu.

Kwa sababu siwezi kukutana na kila mtu. Wanaopata maarifa haya ni wengi na wanaotaka tukutane ni wengi, na pia nina majukumu mengine mengi. Hivyo kuweza kuonana na kila anayetapa tuonane inakuwa vigumu.

Sasa ipo njia moja tu ya mimi kuweza kuonana na kila anayetaka kuonana na mimi. Na njia hiyo ni kuhudhuria semina ya mwaka ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo kwa mwaka huu 2018 itafanyika tarehe 03/11/2018, jijini Dar es salaam. Ada ya kushiriki semina hii ya siku nzima ni tsh laki moja na unaweza kulipa kidogo kidogo mpaka kufikia tarehe ya mwisho ambayo ni tarehe 31/10/2018.

Karibu sana tukutane pamoja kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ambayo itafanyika tarehe 03/11/2018. Kama utashiriki semina hii, fungua kiungo hichi na utaingia kwenye kundi maalumu la wasap la semina hii. Kiungo ni; https://chat.whatsapp.com/L3F4jaeYcZO4drSCxWYrPr

Karibu sana kwenye semina, karibu sana tuonane na kushirikishana yale muhimu kwa mafanikio.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HAKUNA AJALI.

“There are no accidents… there is only some purpose that we haven’t yet

understood.” – Deepak Chopra

pale ambapo mambo ambayo hatutegemei yatokee yanapotokea, huwa tunasema ni ajali. Lakini Chopra anatuambia hakuna ajali, badala yake kuna kusudi ambalo bado hatujalijua.

Kwamba kila kinachotokea kwenye maisha yako, iwe ni kizuri au kibaya, jua kimekuja na kusudi fulani. Hivyo badala ya kushangilia au kulia, unahitaji kukaa chini na kujiuliza hiki kilichotokea, ambacho sikutegemea kama kingetokea, kimekuja na kusudi gani kwangu?

Fanya hivyo kwa kila kinachotokea kwenye maisha yao na hutaona ugumu wowote kwenye maisha, utajifunza na kuwa bora zaidi bila ya kujali umekutana na nini.

Rafiki yangu, hiyo ndiyo dozi yetu ya tano za juma kwa juma namba 33 la mwaka huu 2018. Jifunze, yatafakari maisha yako na jifanyie tathmini ya uhalisia wa maisha yako, je hatua unazochukua zinaendana na kule unakotaka kufika. Kisha chukua hatua sahihi kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Usipoteze fursa nzuri ya kupangilia juma lako namba 34 kabla hujalianza. Muda mchache utakaotenga wa kupangilia juma lako, utaokoa muda wako mwingi sana. Chukua hatua ya kupangilia juma lako kabla ya kulianza na ishi kwa mpango wako huo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji