Moja ya changamoto kubwa kwenye kufikia mafanikio ni kuogopa kufanya maamuzi.
Watu wengi hukwepa kufanya maamuzi kwa sababu wanaogopa kukosea, au wanaona labda wakifanya maamuzi sasa watakosa vizuri zaidi vinavyokuja baadaye.
Wengine hukwepa kufanya maamuzi kwa kujiona bado hawajawa tayari, hivyo kuendelea kuiandaa mpaka pale watakapojiona wamekuwa tayari.
Ukweli ni kwamba, hakuna wakati ambao utajiona umekamilika kwa ajili ya mafanikio. Na pia hakuna wakati ambao utaona umeweza kuchagua kilicho sahihi zaidi kuliko vitu vingine vyote.
Hivyo usikwepe wala kukimbia kufanya maamuzi. Badala yake unahitaji kufanya maamuzi na kuchukua hatua.
Na kama umefanya maamuzi ambayo umekosea, unaweza kurekebisha mbele ya safari. Na hata kama zitajitokeza fursa nzuri zaidi baadaye, ni bora kwenda na kile ambacho umeshafanya maamuzi kuliko kusubiri ambacho huna uhakika nacho.
Kadiri unavyochelewa kufanya maamuzi kwenye jambo lolote, ndivyo unavyokosa nafasi nzuri ya kupiga hatua. Hivyo usiwe mtu wa kukwepa kufanya maamuzi.
Ukishapata taarifa na maarifa unayohitaji, fanya maamuzi mara moja na anza kuchukua hatua.
Ni bora kufanya maamuzi mabaya ambayo unayachukulia hatua, kuliko kutokufanya maamuzi kabisa. Kwa sababu kwa maamuzi mabaya utajifunza na kujua ni makosa gani ya kuepuka wakati mwingine, lakini usipofanya maamuzi kabisa, hakuna chochote utakachojifunza wala hatua utakazopiga.
Amua na chukua hatua, ukigundua kuna kitu hukuwa umejua wakati wa maamuzi, fanya maboresho na endelea mbele.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,