Watu wengi hufikiri maisha ni kufanikiwa au kushindwa, na hivyo hutumia kila namna kukwepa kushindwa, wakiamini kama hawashindwi basi wanafanikiwa.

Na hakuna uongo mwingine duniani unaozidi huo. Siyo kweli kwamba kama hushindwi basi unafanikiwa. Kama hushindwi maana yake hujaribu mambo makubwa, mambo yaliyo nje ya uwezo wako.

Na kama hujaribu mambo makubwa na yaliyo nje ya uwezo wako, huna nafasi ya kutengeneza mafanikio makubwa.

Ili ufanikiwe unahitaji kushindwa zaidi kwa sababu unaposhindwa, unakuwa umejaribu vitu vikubwa na ambavyo hujazoea, hivyo unajifunza na kukua zaidi.

Kama hushindwi, kwa hakika tunaweza kusema unafanya vitu ambavyo umezoea na una uhakika navyo. Na hakuna aliyewahi kufanikiwa kwa kufanya vitu alivyozoea na ambavyo ana uhakika navyo.

Shindwa mara nyingi uwezavyo, na kwa hakika, kushindwa ndiyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kijana mmoja aliyekuwa ameanza kazi kwenye kampuni kubwa alimfuata mkurugenzi wa kampuni na kumuuliza nawezaje kufanikiwa sana kwenye kazi hii? Mkurugenzi bila ya kusita akamwambia hakikisha unashindwa zaidi na zaidi.

Huwezi kukwepa kushindwa kama unataka kufanikiwa kwenye maisha yako. Kwa sababu kushindwa ndiyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kwenye kila kikubwa unachohitaji kufanya kwenye maisha yako, utaanzia sehemu ambayo hujui na huna uhakika nayo.

Kwenye vitu vingi unavyoanza kwenye maisha yako, vingi utakuwa unaanza uongo, yaani mwanzoni utakuwa unajipa moyo hiki ndiyo chenyewe, lakini unapoanza unagundua hukujua vizuri ulichokuwa unataka.

Usianguke wala kukata tamaa pale unaposhindwa kwenye yale unayofanya ili kufanikiwa. Badala yake furahia kwa sababu kushindwa kwako ndiyo darasa muhimu sana kwa mafanikio yako.

Kushindwa ndiyo njia pekee inayokupeleka kwenye mafanikio makubwa, usiikimbie kama unataka mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha