Unapochagua mteja wa biashara yako, na ukaona kabisa ana sifa zote za wateja wa biashara yako. Yaani ana uhitaji ambao biashara yako inaweza kumtimizia na pia anaweza kumudu gharama unayotoza. Kama mteja huyo hatanunua, basi kosa litakuwa lako na siyo la mteja.

Mteja, hasa mpya, hatakuwa tayari kununua kwako mpaka pale utakapompa sababu za kutosha kwa nini anunue kwako, na pia kwa nini anunue sasa.

Mteja ana machaguo mengi ya wapi anunue, kwa sababu biashara yoyote unayofanya, wapo wengi pia ambao wanaifanya.

Mteja pia ana chaguo la wakati gani anunue, na yupo tayari kusubiri zaidi iwezekanavyo akiamini anaweza kupata kilicho bora zaidi na kwa bei nzuri zaidi kwake.

Hivyo wewe kama mfanyabiashara, una majukumu makubwa mawili unapokutana na mteja wako.

Jukumu la kwanza ni kwa nini anunue kwako na siyo kwa wengine. Hapa unahitaji kuwa na kitu cha tofauti, ambacho n cha thamani kwa wateja wako na hawawezi kukipata sehemu nyingine yoyote. Hicho kitawashawishi sana kununua.

Jukumu la pili ni kwa nini anunue sasa na siyo kusubiri mpaka baadaye au siku nyingine. Hapa unahitaji kumpa mteja msukumo na hamasa ya kununua. Unaweza kumpa zawadi kama atafanya manunuzi sasa. Au kuwa na namna nyingine za kumfanya aone thamani kubwa zaidi kwake ni kununua sasa na siyo kusubiri.

Mpe mteja kila sababu kwa nini anunue kwako na anunue sasa, na jua kama mteja hajanunua, kuna kosa umefanya, hivyo jifunze na kuwa bora zaidi wakati mwingine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha