Pamoja na kuwa na mipango mizuri ambayo mtu unaifanyia kazi, matokeo hayatakuja kama ulivyofikiri yanakuja. Kuna vitu vingi sana vitakwenda tofauti na unavyotegemea wewe.

Pamoja na kujua kwamba vitu vitakwenda tofauti, pamoja na kujua kwamba kuna uwezekano ukawa umekosea na pia upo uwezekano wa kushindwa, kuna kosa moja kubwa sana unalopaswa kuepuka kwenye mipango na utekelezaji wa mipango yako.

Kosa hilo ni kuonesha hali ya wasiwasi kwamba kile unachofanya kinaweza kisitoe matokeo sahihi, au unaweza kuwa umekosea. Ukishaonesha hali ya wasiwasi, unapunguza kujiamini na hata wale wanaokuzunguka nao wanapunguza kukuamini.

Kinachotokea ni hamasa ya kila mtu inashuka na hakuna hatua kubwa ambayo watu wanapiga.

Huhitaji kuonesha hata chembe ya wasiwasi kwamba kinachofanyika kinaweza kisiwe sahihi au hakitaleta matokeo mazuri. Unahitaji kuweka imani yako yote kwenye kile ulichopanga na kwenye hatua unazochukua. Na hata wale wanaokuzunguka, wale unaowategemea wakusaidie, watakuwa na uhakika na hamasa ya kufanya zaidi.

Ni bora kukosea ukiwa unajiamini na huna wasiwasi, kuliko kuwa sahihi lakini una wasiwasi na kutokujiamini. Kwa sababu wasiwasi na kutokujiamini hakutakuacha uchukue hatua yoyote. Lakini unapojiamini, utachukua hatua, na hata kama utakosea, utaweza kufanya marekebisho baadaye.

Unapaswa kuwa makini sana na hili pale unapokuwa unaongoza wengine, au kuna watu wanaokuangalia wewe kama mfano kwao. Ukionesha dalili zozote za kuwa na wasiwasi kwamba hatua fulani haitaleta matokeo watu wanayotaka, wasiwasi huo utasambaa kwa kasi kama moto kwa wote unaowaongoza na utashangaa hakuna mwenye msukumo wa kuchukua hatua.

Weka mipango na anza kuchukua hatua, ukiamini hiyo ndiyo mipango sahihi na unazochukua ndiyo hatua sahihi kabisa kwa sasa. Kama utahitaji kubadili fanya hivyo, lakini kamwe usiwe na wasiwasi kwamba mpango ulionao au hatua unazochukua hazitaleta matokeo unayotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha