Rafiki yangu mpendwa,

Kadiri dunia inavyopiga hatua, ndivyo watu wanavyokuwa wavivu, ndivyo watu wanavyokwepa kazi na kuwa na sababu nyingi za kwa nini wasifanye kazi muda mrefu.

Siku hizi kila mtu amekuwa akizungumzia mlinganyo sahihi kwenye maisha, ambapo muda wa kazi na muda wa kupumzika unapaswa kuwa kwenye mlinganyo.

Na wengine wamekuwa wanayagawa masaa 24 ya siku kwenye makundi matatu, masaa nane ya kazi, masaa nane ya kupumzika na kufanya yale ambayo ni muhimu kwa mtu lakini siyo kazi na masaa mengine nane ya kulala.

Lakini tukiangalia haya yote, yanaletwa na maendeleo ambayo yanatokea duniani.

Tukiangalia miaka ya nyuma, watu walikuwa hawana anasa ya kugawa muda wa kufanya kazi, kupumzika na kulala. Watu walikuwa wanafanya kazi kulingana na uhitaji walionao, na pale kazi inapoisha basi walipata nafasi ya kupumzika.

Chukua mfano wa jamii ya wakulima, kama ni kipindi cha kupanda mazao, unafikiri mtu alienda shamba na kusema nitapanda mazao na masaa nane yakiisha nitaacha, au nitapanda jumatatu mpaka ijumaa na wikiendi nitapumzika? Haikuwa hivyo, watu walifanya kazi kulingana na uhitaji wake mpaka inapokamilika.

5c821-fanya2bkazi

Mengi sana yamekuwa yanasemwa kuhusu kazi, na wengi wanaendelea kudanganyana sana kuhusu kazi. Wapo wanaoambiana kwamba huhitaji kutumia nguvu kwenye kazi, bali unahitaji kutumia akili. Lakini huo ni uongo, tumia akili uwezavyo, lakini bila nguvu, tena nguvu za maana, hakuna hatua mtu ataweza kupiga kwenye kile anachofanya.

Rafiki yangu, leo ninataka nikushirikishe kitu kimoja muhimu sana kuhusu mlinganyo unaotafuta kwenye maisha yako.

Na nitaanza kwa kukuuliza kitu kimoja, je umewahi kwenda dukani kununua kitu ambacho unapimiwa kwa kilo? Umewahi kwenda kununua sukari kilo moja? Na je umewahi pia kwenda kununua sukari kilo mbili au kilo tano?

Je unapoenda kununua sukari hiyo, muuzaji anafanya nini? Ukienda kununua kilo moja, muuzaji anachukua jiwe la kilo moja na kuweka kwenye mizani, kisha anaweka sukari upande wa pili mpaka ilingane na jiwe la kilo moja. Kadhalika ukitaka kilo mbili, ataweka jiwe la kilo mbili kisha kuweka sukari mpaka ilingane na jiwe la kilo mbili.

Hicho ndiyo kikubwa sana ambacho nataka uelewe kuhusu mlinganyo kwenye maisha yako.

Kwamba dunia inakupa sawasawa na unavyotoa, ila utoaji wako ni kwenye kazi. Kama ambavyo utapata wingi wa sukari kulingana na ukubwa wa jiwe, mafanikio yako yatatokana na ukubwa wa kazi unayofanya.

SOMA; Tukumbushane Ustaarabu Wa Zama Hizi (Mambo Kumi Muhimu Ya Kuzingatia Katika Zama Hizi Ili Uweze Kufanikiwa).

Kama unataka mafanikio makubwa, maana yake unahitaji kuweka juhudi kubwa zaidi na kwa muda mrefu zaidi kwenye kazi unayofanya.

Kadiri unavyotoa zaidi kwa upande wa kazi, ndivyo unavyopokea zaidi kwa upande wa matokeo na mafanikio.

Hivyo kama kuna mlinganyo unaotafuta kwenye maisha yako, unahitaji kuweka kazi zaidi na siyo kutafuta mapumziko zaidi.

Na kama unaona kazi unayoifanya ni ngumu kwako na unahitaji kupata mapumziko zaidi, kuna mambo mawili hapo. Labda huna ndoto kubwa unazofanyia kazi na ambazo zinakusukuma zaidi. Au hupendi kile unachofanya.

Mwanafalsafa mmoja amewahi kusema, unapaswa kufanya kile ambacho unakipenda kiasi kwamba huhitaji kupumzika, kwa sababu kufanya kitu hicho ni mapumziko tosha. Kwamba kufanya kazi na kucheza kunakuwa ni kitu kimoja.

Rafiki, ninachokuambia hapa ni kimoja, jitoe zaidi kwenye kufanya kazi kama unachotaka ni mafanikio makubwa. Achana na wale ambao wanatenga muda wa kazi na muda wa kupumzika, ambao wanataka mapumziko kila mwisho wa wiki na wanaona kazi kama ni mzigo kwao. Hakuna anayeweza kufanikiwa kwa kukwepa kazi. Penda kazi, jitoe kwa ajili ya kazi na utafika popote unapotaka kufika. Kwa sababu dunia ipo tayari kukupa sawasawa na unavyotoa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji