Pata picha ya mkulima huyu,
Ameambiwa akilima karanga zitamlipa sana, analima shamba na kupanda karanga, wakati karanga zinaanza kuchipua, anaambiwa kuna fursa mpya, kama atalima mahindi, basi atafanikiwa sana, anang’oa karanga na kupanda mahindi. Mahindi yanakua na kabla hayajafikia kuvunwa, anaambiwa fursa kubwa sasa hivi ni maharagwe, anang’oa mahindi hayo na kupanda maharagwe.
Ni jina gani rahisi unaweza kumwita mkulima wa aina hiyo? Ukimwita mpumbavu unakuwa hujakosea sana. Maana ni mpumbavu pekee ambaye anaweza kuhangaika na kilimo kiasi hicho. Ni mpumbavu pekee asiyejua kwamba huwezi kunufaika na kilimo kama huna subira ya kupanda mpaka kuvuna.
Kwenye kilimo wengi hawafanyi hivyo, lakini inapokuja kwenye biashara, ni kama kitu cha kawaida kabisa. Watu wengi wanajaribu kila aina ya biashara, halafu wanakuambia nimeshafanya kila kitu lakini sifanikiwi.
Ukiangalia kila biashara ambayo wamejaribu, hakuna hata moja ambayo wamekaa nayo muda mrefu, wakaweka kazi, wakajifunza na kuweza kupiga hatua zaidi.
Zote wanaanza na wanapokutana na changamoto, wanakimbilia kwenye biashara nyingine.
Huu ugonjwa wa kukimbizana na kila aina ya fursa mpya ni ugonjwa mbaya sana kwa ukuaji wa biashara.
Chagua nini unataka kwenye maisha yako, na chagua biashara ambayo unaweza kuifanya muda wote bila ya kujali nini kinaendelea kwenye maisha yako. Kisha weka juhudi kwenye biashara hiyo, na ondokana kabisa na mchezo wa kukimbizana na kila aina ya fursa.
Kila kitu kinalipa kama utaweka juhudi, uvumilivu na ung’ang’anizi. Usidanganyike na fursa mpya zinazoibuka kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,