Kama umewahi kuwaangalia wanyama jinsi wanavyoishi, basi utakuwa umeiona siri kubwa ya namna asili inavyopeleka mambo yake.
Chukua mfano wa simba ambaye amemwona swala anapita, kisha akaanza kumkimbiza swala yule, swala akatimua mbio sana, simba akakazana. Lakini pamoja na jitihada zote, swala anafanikiwa kumponyoka simba.
Je unafikiri simba anafanya nini baada ya hapo? Unafikiri simba anajiambia hana bahati kwa sababu amemkosa swala? Unafikiri simba atakaa chini na kuanza kufanya tathmini ni kwa namna gani pori halijakaa vizuri na ameshindwa kumkamata swala?
Unafikiri simba ataanza kulalamika na kulaumu kwa nini hajamkamata swala? Na je unafikiri simba atajiambia mimi siwezi tena kukamata swala na kuanzia sasa sitakimbizana tena na swala?
Hayo siyo yanayotokea, maana sivyo simba wanavyoishi maisha yao. Simba akimkosa swala mmoja anatafuta mwingine wa kumkimbiza mpaka ampate. Kwa sababu maisha yake yanategemea kula na asipokula hakuna maisha.
Kadhalika kwa wanyama wengine, kuanzia kuku mpaka sisimizi, kila mmoja anakazana kila siku kuhakikisha anapata chakula na maisha yake yanaenda. Akikosa hakai chini na kulalamika, badala yake anakuwa bize kutafuta chakula.
Hivi pia ndivyo sisi tunapaswa kuendesha maisha yetu, siyo kwa kulalamika na kukata tamaa pale tunaposhindwa au kukosa tulichotaka. Badala yake kuendelea kuweka juhudi.
Ukishindwa au kukosa ulichotaka, usikae chini na kuanza kujilaumu au kujiambia huwezi, badala yake unahitaji kuwa bize kwenye kuchukua hatua zaidi mpaka upate unachotaka.
Hivi ndivyo asili inavyofanya kazi, nawe ukipeleka maisha yako hivyo, hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,