Hadithi za mafanikio ya wengine huwa haziwasaidii wengi kwa sababu hadithi hizi zinaonesha matokeo na siyo mchakato.

Utaambiwa mtu alianzia hapa na sasa amefika pale, alianzia chini kabisa na ameweza kufika juu sana.

Mchakato huwa hauelezwi kwenye hadithi hizi, na hata ukimuuliza mtu aliyefanikiwa sana akueleze mchakato wake, kuna vitu vingi hataweza kukueleza.

Maana kuna vitu vingine vinatokea kwenye maisha yake na yeye mwenyewe hana uhakika aliviwezaje. Pia kuna aina ya bahati fulani ambazo mtu anakutana nazo kwenye safari yake ya mafanikio, ambazo anaweza asikuambie bahati za aina hiyo.

Unapoyaangalia mafanikio, usikazane sana na matokeo, kazana na mchakato.

Angalia hatua ambazo utapiga kila siku, juhudi utakazoweka kila siku, namna unavyokuwa bora zaidi kila siku.

Mchakato wa kila siku ndiyo utakujenga kwa ajili ya mafanikio zaidi. Na siyo kuyaangalia matokeo pekee. Matokeo ni mazuri kwa kukupa hamasa, lakini hamasa ni asilimia moja ya mafanikio. Asilimia 99 ni juhudi unazoweka, ambazo utaziweka kwa muda mrefu kabla hujaona matokeo makubwa unayotegemea kupata.

Mafanikio yapo kwenye mchakato, matokeo ni kile ambacho wengine wanaona kwa nje. Kazana zaidi na mchakato.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha