Rafiki yangu mpendwa,

Tunaishi kwenye dunia ambayo ufanyaji wa kazi unapigwa vita na kila mtu. Nimekuwa naona mijadala kwamba matajiri wakubwa wa dunia wanapendekeza watu wawe wanapewa kipato cha kuendesha maisha yao hata kama hawafanyi kazi. Ni kitu ambacho kwa haraka kinaweza kuonekana ni kuwasaidia wenye shida, lakini baada ya muda kitakuwa na madhara makubwa sana kwa jamii nzima kwa ujumla.

Pia wapo wale wanaosema huhitaji kutumia nguvu, bali kutumia akili tu kwenye kazi. Wana maneno yao ya kiingereza, DON’T WORK HARD, WORK SMART. Hapa wengi wamedanganyana sana na fursa zisizo sahihi, wakaishia kupoteza muda wao na fedha zao pia.

Na wenye balaa zaidi ni wale wacheza kamari, ambayo siku hizi wameipa jina la ubashiri wa matokeo, na pia wale wanaocheza bahati nasibu zinazoibuka kila siku. Ambapo watu wanashawishiwa na kuhakikishiwa kabisa kwamba kwa kutumia shilingi mia tano, na bila ya kufanya kazi yoyote wanaweza kupata mamilioni ya fedha. Na watu wanakazana sana.

Ukiangalia namna jamii inavyoenda, utaona kabisa kwamba kila mtu anapigana vita dhidi ya kazi. Kila mtu anaona kufanya kazi ni kubaya, ni kupoteza maisha, ni kujitesa na fikra nyingine ambazo zimepandikizwa kwa watu.

Kwa wale walioajiriwa, kiwango cha kufanya kazi ni masaa 8 kwa siku, siku tano au sita kwa wiki ambapo jumla kwa wiki yanakuwa masaa 40 mpaka 50. Wengi bado wanaona muda huu ni mwingi sana. Na baadhi ya nchi na hata makampuni makubwa, yameanza kupunguza muda huo wa kazi.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Ninachokuambia rafiki yangu, na ambacho nimekuwa nakuambia mara zote, kama unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako, lazima uende kinyume kabisa na namna jamii inavyochukulia kazi.

Jamii inachukia kazi, wewe unahitaji kuipenda sana. Jamii inakazana kupunguza muda wa kazi wewe unahitaji kuuongeza zaidi. Jamii inasema usifanye kazi kwa nguvu, tumia akili, wewe fanya kazi kwa nguvu na kwa akili pia.

Unahitaji kuipenda kazi mno, unahitaji kuweka muda mwingi kwenye kazi yako, unahitaji kuweka juhudi kubwa kwenye kazi yako. Na kama wanavyosema kazi haimtupi yule anayeipenda.

Lakini sasa tunarudi kwenye uhalisia, kupenda kazi na kuweka muda mwingi kwenye kazi yako siyo kitu rahisi, hasa ukizingatia unahitaji kuwa na maisha mengine nje ya kazi.

Na hapo ndipo ninapotaka kukusaidia leo, leo nataka kukupa njia ya kukuwezesha wewe kufanya kazi zaidi ya wengine na kuweza kufanikiwa sana.

SOMA; Kama Unatafuta Mlinganyo Sahihi Kwenye Maisha Yako, Kuna Kitu Hiki Muhimu Sana Unapaswa Kukijua.

Njia hiyo ni kupenda sana kile unachofanya, kukijali hasa na kufanya kazi yako kuwa maisha yako. Kama unapenda sana kile unachofanya, huna haja ya kutenga muda wa maisha na muda wa kazi. Kazi yako inakuwa maisha yako na maisha yako yanakuwa kazi yako. Utakuwa huna haja ya kusema upumzike, maana kazi yako ni mapumziko tosha kwako.

Hupaswi kutenganisha kazi yako na maisha yako, hupaswi kutenga muda wa kazi na muda wa maisha. Kama unachofanya ni kile unachojali hasa, ambacho ungeweza kufanya hata kama hulipwi, basi unahitaji kufanya.

Watu wote waliofanikiwa sana, hawafanyi kazi, bali wanafanya kile wanachopenda kufanya. Na hivyo hawahesabu ni masaa mangapi wamefanya kazi au juhudi kiasi gani wameweka. Wao wanafanya kazi kwa namna walivyopanga kufanya, na wanafanya kwa kiwango wanachoona kinafaa.

Penda sana kile unachofanya, jali sana kile unachofanya, na hutahitaji kusumbuka na wale wanaohesabu muda wa kazi au juhudi wanazoweka. Utafanya kazi kwa kiasi kinachohitajika na utafanikiwa sana kupitia kazi yoyote ile unayofanya.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha