Jina lako, yaani ile sifa ambayo wengine wanayo juu yako, ndiyo rasilimali muhimu sana unayomiliki kwenye maisha yako.

Hii ndiyo rasilimali pekee ambayo hakuna mtu anayeweza kukuibia, na pia hakuna mtu anayeweza kuiiga kwa namna ilivyo.

Ndiyo kitu pekee kinachoweza kukutofautisha wewe na wengine wote hapa duniani.

Swali ni je jina lako limebeba nini?

Jina lako linapotajwa mbele ya wengine, wakati wewe haupo wanapata taswira gani?

Najua unajua kuna jina la mtu likitajwa unapata picha ya ulevi wake, au utapeli wake, au wizi wake.

Sifa ya jina inatokana na zile tabia ambazo mtu anazionesha kwenye maisha yake. Na hutaweza kuwalazimisha watu wakuchukulieje, bali wao wenyewe wataamua kukuchukulia kwa namna unavyojiwasilisha kwao.

Hivyo basi rafiki yangu, jenga jina ambalo litakuwakilisha wewe vizuri kwa wengine. Wafanye watu wasipate ugumu kukutambulisha kwa wengine, hata kama haupo. Wafanye watu waweze kueleza sifa yako na ikawa rahisi watu kukujua.

Julikana kwa uchapaji kazi usio wa kawaida, kwa namna unavyopenda kile unachofanya na kukifanya kwa kwenda hatua ya ziada.

Julikana kwa kuwa mtu mwenye mipango na ambaye unatekeleza kila unachopanga kufanya na siyo kuahirisha.

Julikana kama mtu ambaye anajali sana muda wake, asiyepoteza hata dakika moja ya muda wake kwa mambo yasiyo muhimu.

Julikana kama mtu ambaye akitoa neno lake basi inakuwa sheria kwake, anatekeleza kile anachoahidi na siyo mbabaishaji.

Julikana kama mtu ambaye anajali na kuheshimu kila mtu bila ya kujali umri, cheo au hadhi yake.

Kwa kutengeneza jina lako kwa njia hii, kila mtu atataka kufanya kazi na wewe, kila mtu atataka kununua chochote unachouza na mafanikio hayatakuwa magumu kwako.

Tengeneza na linda sana jina lako, hiyo ndiyo rasilimali pekee unayomiliki hapa duniani inayoweza kukupa chochote na ambayo hakuna anayeweza kukunyang’anya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha