Siku mpya,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUITAWALA DUNIA…
Kama unataka kuitawala dunia, kuna kitu kimoja pekee unachopaswa kukitawala hapa duniani, kitu hicho ni akili yako mwenyewe.
Ukiweza kutawala akili yako, ukadhibiti fikra zako zikaenda vile unavyotaka wewe na siyo kama dunia inavyotaka ufikiri, ukiweza kujijengea mtazamo unaotaka wewe na siyo ule ambao dunia inataka uwe nao, utaitawala hii dunia vizuri sana.

Kama unataka kuwatawala wengine, kuna mtu mmoja ambaye unapaswa kumtawala. Mtu huyo ni wewe mwenyewe. Ukiweza kujitawala wewe mwenyewe, ukajisimamia kwa nidhamu ya hali ya juu, ukajiadhibu pale unapokwenda kinyume na nidhamu unayojijengea, utaweza kuwatawala wengine.

Wengi wanakazana kuitawala dunia wakati hawawezi hata kuianza siku yao kwa mawazo yao wenyewe. Wataianza siku na habari, umbea, udaku na mitandao ya kijamii. Hakuna matumizi mabaya ya akili kama hayo.

Wengine wanakazana kuwatawala wengine wakati wao wenyewe hawawezi kupanga ratiba walizojiwekea. Mtu anajiambia ataamka asubuhi, au ataweka akiba, na hawezi kutimiza vitu rahisi kama hivyo, lakini anataka atawale wengine, anaishia kusumbuka sana.

Tawala akili na fikra zako, jitawale wewe mwenyewe kwa kujijengea nidhamu na kujiadhibu, na dunia nzima itakuwa chini yako, bila hata ya kutumia nguvu kubwa kuitawala dunia.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutawala akili yako, mwili wako na hisia zako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha