Kuna watu wengi wanaingia kwenye biashara wakiwa wameshajiandaa kushindwa.
Wanaingia kwenye biashara wakiwa hawana kitu cha tofauti wanachokwenda kuuza.
Wanauza kile ambacho kila mtu anauza, na kwa namna ambayo kila mtu anauza.
Sasa swali ni kama kile unachouza mteja anaweza kukipata sehemu nyingine yoyote, kuna umuhimu gani wa wewe kuwepo?
Ipo sheria inasema kama vitu viwili vinavyofanana vipo sehemu moja, kimoja hakina umuhimu.
Kadhalika kwa biashara yako, kama hauwezi kuuza kitu ambacho wengine hawauzi, au kuuza kile wanachouza kwa namna tofauti kabisa, huna umuhimu wa kuwepo kwenye biashara.
Utaishia kusumbuka na hata kusumbua wengine.
Chagua kuuza kitu ambacho wengine hawauzi, na kama unauza kinachouzwa na wengine, basi ambatanisha huduma ambayo mteja wako hawezi kuipata sehemu nyingine ila kwako tu.
Kufanya tofauti na hapo ni uvivu kibiashara, na hakuna kitakachokuondoa kwenye biashara kwa haraka kama uvivu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,