“This is a fundamental irony of most people’s lives. They don’t quite know what they want to do with their lives. Yet they are very active.”— Ryan Holiday

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNAKIMBILIA WAPI?
Jambo la kushangaza kuhusu maisha ya wengi ni kwamba hawajui nini hasa wanachotaka kwenye maisha hao, lakini wapo bize kweli kweli.
Wengi hawana ndoto yoyote kubwa kwamba miaka kumi ijayo watakuwa wapi, lakini leo watakuambia hawana muda.

Kama hujui wapi unapomwenda, njia yoyote itakayojitokeza mbele yako itakuwa sahihi kwako.
Na kama hujui unapokwenda, njia yoyote utakayoifuata itakupoteza.
Haina maana yoyote kwenda kasi wakati hujui unakokwenda, kwa sababu utazidi kupotea.

Hitaji lako la kwanza kabisa ni kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako, wapi unataka kufika, nini unataka kufanya na alama gani unataka kuacha hapa duniani.
Ukishajua hayo, sasa unaweza kwenda kasi utakavyo na kupuuza yale yasiyohusika na unachotaka.

Lakini kama hujajua kule hasa unakokwenda, kila siku utakuwa unasumbuka na kila aina ya fursa mpya.
Leo utaambiwa hiki kinalipa, unaingia,
Kesho unaambiwa achana na hicho, kuna kingine kinalipa zaidi, unaacha cha mwanzo na kuingia kingine.
Kila siku unakuwa bize, kila siku unachoka, lakini miaka inapita na huoni hatua zozote ulizopiga.

Kama hujaamua nini hasa unataka na maisha yako, nini hasa upo tayari kusimamia hata kama utakutana na ugumu na kushindwa, ubize wowote ulionao sasa ni ubatili mtupu.
Unajifurahisha tu, lakini majuto yatafuata baadaye.

Fanya maamuzi muhimu sana ya maisha yako ya nini unataka kufanya na wapi unataka kufika kisha simamia maamuzi hayo, ije mvua, lije jua.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa bize kwenye kile hasa ulichoamua kwenye maisha yako na siyo kwa kufuata mkumbo.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha