Ni bure, yaani hakuna.
Kwa kifupi, hakuna thamani unayoipata kwenye ushauri wa bure, ambayo hukuwa unaijua tayari.
Kwa sababu wengi wanaokupa ushauri wa bure kwenye biashara, wanaongelea vitu ambavyo tayari vimezoeleka, au wameona au kusikia kwa wengine.
Hakuna mtu anayeweza kukupa ushauri wa bure kwenye biashara, ambao umetokana na utafiti wa kina uliofanyika kwenye biashara nyingine.
Ni rahisi mtu kukuambia ungeuza hiki au ungeuza kile basi ungepata faida sana. Ni rahisi mtu kukuambia ungepunguza bei au kuongeza bei ungepata faida sana.
Lakini mtu kuijua biashara yako kwa undani, na kujua wapi inakwenda miaka kumi ijayo, kisha kukupa ushauri ambao utaiwezesha biashara hiyo kuwa imara zaidi miaka kumi ijayo kuliko sasa, ni kazi ngumu, na huwa haiji bure.
Lakini pia nikukumbushe, kila ushauri una gharama yake, na ushauri wa bure hutalipia mpaka pale utakapoanza kuutumia. Kwa sababu utakuharibia biashara yako kiasi kwamba utakuwa umeulipia kwa gharama kubwa.
Hoji sana kila aina ya ushauri unaopata kuhusu biashara yako, mwisho wa siku wewe ndiye utakayebeba mzigo wa biashara yako, wewe ndiye unayejua miaka 10, 20 na hata 50 ijayo unataka biashara hiyo iwe wapi. Na pia kumbuka, makosa yoyote utakayofanya kwenye biashara yako, wewe ndiye utakayefanya kazi ya kuyarekebisha.
Mara zote jikumbushe ndoto yako kubwa kibiashara, na angalia njia bora zaidi kwako kufikia ndoto hiyo, na kuwa makini sana na kila aina ya ushauri unaopokea. Sehemu kubwa ya ushauri ambao watu wanakupa bure kabisa, ni sumu kwa biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,