Ni kutengeneza wateja wa biashara hiyo.

Kutengeneza sifa ambayo wateja wako wanakuwa nayo kuhusu wewe.

Huwezi kwenda kununua kitu kwenye biashara mara moja na ukatoka hapo ukawaambia watu ile ni sehemu nzuri. Utaenda na kupata huduma nzuri, utashawishika tena kurudi na utapata huduma nzuri, mara ya tatu ukipata tena huduma nzuri, unajijengea imani kwamba ile ni sehemu sahihi.

Hata yeyote anapokuuliza sehemu gani ya uhakika, unawaelekeza pale, kwa sababu mara zote umekwenda pale, umepata huduma bora.

Hivyo kwenye biashara yako, juhudi kubwa kabisa ni kutengeneza wateja wanaoiamini biashara hiyo. Wateja ambao wanaweza kusema mbele ya wengine bila ya wasiwasi kwamba wakija kwenye biashara yako watapata kile wanachotaka.

Zoezi hili ni gumu pale unapoanza biashara, kwa sababu hakuna mwenye historia ya kupata huduma nzuri kutoka kwako. Hivyo wengi wanaonunua mwanzoni ni kama wanajaribu tu.

Na hapa ndipo unapokuwa na jukumu kubwa zaidi na kuhakikisha kila anayejaribu basi ananasa. Yaani mtu akinunua kwako mara moja, basi anatamani kurudi tena na tena na tena.

Toa huduma bora na kuwa na kiwango cha huduma kinachokwenda juu na siyo chini. Kila mteja anayeridhika na huduma unayotoa, ni njia bora ya kutangaza zaidi biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha